Wananchi watakiwa kufanya kazi kwa bidii, kuwaenzi waasisi wa Taifa

Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji, akizungumza na Watumishi na baadhi ya Wananchi wa wilaya hiyo, waliojitokeza kuadhimisha  miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, maadhimisho yaliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa ulioko Manispaa ya Moshi.

MOSHI-KILIMANJARO.

Serikali Wilayani Moshi mkoani Kilimanjro, imewataka wananchi, kuwajibika kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuwaenzi Waasisi wa Taifa, akiwemo Mwasisi wake Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wito huo umetolewa Desemba 9,2024 na Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji, wakati akizungumza na watumishi na baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo, waliojitokeza kufanya shughuli za kijamii ikiwa ni kuitikia wito wa Rais Dk. Samia  Suluhu Hassan wa kufanya shughuli za kijamii kama sehemu ya Maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Amesema wakati Watanzania wakiadhimisha  miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, yako maendeleo makubwa ambayo wananchi wakiyashuhudia huku msingi wake, uliwekwa na viongozi pamoja na wananchi wakati wa kupata Uhuru, ambapo waliwajibika ipasavyo hivyo watumishi na wananchi kwa ujumla hawana budi kuwajibika ili wale wanaokuja nyuma walikute Taifa likiwa na maendeleo ambayo na wawo watawajibika kuyaendeleza.

Aidha mkuu huyo wa Wilaya litoa rai kwa wananchi kuwapuuza wale wanaobeza maendeleo yaliyopatikana tangu Uhuru kutokana na ukweli yanaonekana wazi na ambayo pia wenyewe (wanaobeza) wananufaika nayo.

Amesema mfano mzuri ni maboresho yaliyoko kwenye sekta za afya, elimu, miundombinu mizuri ya barabara na maji safi na salama; hayo yote ni ushahidi tosha wa maendeleo yaliyopatikana kwa miaka 63 iliyopita.

Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini Faraji Swai, amesema yako maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hususan katika sekta ya elimu, ambapo kwa Manispaa ya Moshi, ilikuwa na shule moja tu ya sekondari ya Mawenzi, lakini kwa sasa kila Kata inayo shule ya sekondari.

Akiwasilisha mada kama sehemu ya maadhimisho hayo ambayo majumuisho yake yalifanyika katika Uwanja wa Mashujaa ulioko Manispaa ya Moshi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Uhsirika Moshi, (MoCU) Dk. Jonas Kaleshu, amesema kuwa Tanzania ni moja ya Mataifa machache ya Afrika ambayo yamepata mafanikio makubwa tangu kupatikana kwa Uhuru.

"Wakati nchi ya Tanzania inapata Uhuru mwaka wa 1961 kulikuwa na Wahandisi wawili tu, ambapo kwa leo wako  maelefu ya Wahandisi katika fani mbalimbali, watumishi wa serikali walikuwa 403 na leo hii wako zaidi ya 30,000 wakati mauzo ya nje yalikuwa yenye thamani ya Dolla za Marekani Sh milioni 115 hadi kufikia Aprili mwaka, huu mauzo hayo yamefikia zaidi ya dolla za marekani Sh bilioni 14.5.

Akiongea katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe, amesema kuwa watumishi wa taasisi mbalimbali walishiriki katika maswala ya usafi ikiwemo kwenye makuburi ya Karanga yaliyo Manispaa hiyo.

Naye Amon Safieli kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Moshi vijijini,  amesema mbali na shughuli za usafi zilizofanyika maeneo mbalimbali ya Moshi Vijijini, pia watumishi na wananchi wengine walishiriki shughuli za michezo ambazo zilienda sambamba na mashindano ya michezo aina mbalimbali.








 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.