MOSHI-KILIMANJARO.
Mabaraza ya wafanyakazi, yametakiwa
kutumika kama chombo muhimu katika kuboresha na kuimarisha demokrasia kwenye
eneo la kazi, badala ya kutumika pekee kukusanya na kupitia maoni ya watumishi.
Mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi, Idara ya Uhamiaji Taifa (TUGHE) Joel George Kaminyoge, aliyasema
hayo Desemba 10,2024, wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi, Idara ya
Uhamiaji, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda
(TRITA) Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema kuwa mabaraza hayo
yanahusisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya taasisi au shirika
wanamofanyia kazi, jambo ambalo huongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji mahala pa kazi.
“Zamani mabaraza haya ya
wanyakazi yalikuwa ya kiharakati sana, na ndio maana kulikuwa na migogoro mingi
kati ya wafanyakazi na waajiri ambayo, ilikuwa haiishi, lakini kwa sasa hivi sivyo, kwa sababu tunakaa
kwenye meza moja na kukubaliana kati ya waajiri na wafanyakazi na hivyo kumekuwepo
kwa mafanikio makubwa zaidi, ukilinganisha na huko tulikuwa zamani.”amesema Kaminyoge.
Aidha amewataka watumishi
wa umma, kuhakikisha kwamba wanapunguza, kutumia simu janja wanapokuwa kazini
ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi nchini.
Amesema kumekuwa na
malalamiko mengi kwa wahudumu kwa baadhi ya taasisi za serikali kushindwa
kuwahudumia wananchi vizuri kutokana na matumizi yaliyopitiliza ya simu janja.
“Masuala ya kutumia muda
mwingi kuchati kwenye simu, sisi kama Tughe tunasema hapana, wanachama wetu
wanatakiwa kuwajibika, ili kuongeza tija, ukiwa unahitaji kulipwa vizuri
mshahara wako, utahitaji kulipwa vizuri baada ya kufanya kazi kwa bidii na hivyo kuongeza
pato,”amesema.
Mbali na hilo Kaminyonge
amesema wakati ambao Tughe inaadhimisha
miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1994 imepitia mabadiliko mengi
ambayo yamekuwa na tija ikiwemo ujenzi wa watumishi mahali pa kazi.
“Miaka 30 ya Tughe kwangu
mimi ni mafanikio makubwa na miongoni mwa hayo, ni kuwepo kwa mabaraza mawili
ya wafanyakazi mahali pa kazi, ndio yanayowezesha kuwakutanisha kwa pamoja kati
ya waajiri na wafanyakazi, kukaa pamoja, kupanga mipango ya taasisi lakini pia
kuongeza mshikamano na ufanisi mahala pa kazi na ndio maana huwezi kusikia kuna
migogoro katika eneo letu,”amesema.
Kwa upande Kaimu Mwenyekiti
wa Baraza la Wafanyakazi Idara ya Uhamiaji Kamishna Gerald Kihinga, amesema
wakati Tughe inaadhimisha miaka 30 tangu
kuanzishwa kwake, yako mafanikio makubwa ambayo inajivumia kwa kipindi chote
hicho ikiwemo ukamilishaji wa majengo yaliyokuwa hayajakamilika, pamoja na
ufungaji wa mifumo.
Aidha katika Kikao hicho
kilichowakutanisha wanachama wa TUGHE, Idara ya Uhamiaji kote nchini katika
kujadili Bajeti ya Idara ya Uhamiaji kwa mwaka wa fedha 2024/25 wamekumbushwa
kuhusu kuendelea kujikinga na maradhi yanayoambukizwa kwa kujamiiana ili
kuijenga Tanzania ni lazima watumishi wawe na afya njema.
Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi 2004 na Sheria ya Taasisi za Kazi 2004 zinatoa haki kwa wafanyakazi wote kujiunga na vyama vya wafanyakazi na kwa waajiri kuunda vyama vya waajiri kwa maslahi mapana ya ujenzi wa nchi.












