Mangi mkuu wa Machame Gilbert
Shangali, anatarajiwa kusimikwa Desemba 14,2024
MOSHI-KILIMANJARO.
Mkuu wa Mkoa wa Kiliamnajro Nurdin Babi, anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi katika tukio la kusimikwa kwa Mangi mkuu wa Machame Gilbert
Shangali, litakalofanyika Desemba 14, mwaka huu, kijiji cha Machame Wari,
Wilaya ya Hai mkoani humo.
Hayo yamesemwa Desemba 9,2024 na Mwenyekiti wa
Kamati ya maandalizi, Clement Andrea Shangali, wakati akizungumza na waandishi
wa habari mjini Moshi, ambapo amesema kuwa, ni sehemu ya kuendeleza mila na
desturi za Wachaggawa eneo la Machame.
Aidha Mwenyekiti huyo wa kamati ya maandalizi Clement
Andrea Shangali, amesema maandalizi ya kumsimika Mangi Gilbert SHangali,
yameshakamilika, ambapo Mwenyekiti Mstaafu wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT)
Frank Mareallle, atafanya shughuli hiyo ya kumsimika kimila, ambapo tukio hilo litaanza majira ya saa tatu asubuhi, huku
akitoa wito kwa wananchi kuhudhuria kwa wingi kushuhudia tukio la kusimikwa kwa
Mangi mpya wa Machame.
Amesema katika tukio hilo pia kutakuwepo na machifu
wengine kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, Wabunge,
Madiwani, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania mkoa wa
Kilimanjaro (JMT) Jones Mola, Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji, pamoja na
viongozi wa madhehebu ya kidini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ukoo Dk. Harold
Shangali, amesema kuteuliwa kwa Gilbert Shangali, kuwa Mangi wa Wana Machame,
anayo nafasi kuwa ya kuhakikisha kwamba anakwenda kusimamia maadili
ambayo kwa kiasi kikubwa yameporomoka katika jamii.
Aidha Dk. Shangali, amesema machifu wana
mchango mkubwa katika kulinda maadili na kutatua changamoto za kimaadili katika
jamii licha ya kuwa yanashughulikiwa katika ngazi ya serikali.
Naye Katibu wa Umoja wa Machifu mkoa wa
Kilimanjaro Joseph Mselle, amesema Afrika ilikuwa na mfumo wake wa utawala,
uliokuwa unarithishwa kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Akizungumzia tawala za jadi katika nchi ya
Tanzania Mselle; amesema ni alama ya mfumo wa kiuongozi kwa Waafrika kabla ya
ukoloni kitu ambacho ndicho kilikuwa ni kielelezo cha kutambulisha tamaduni
zetu.
Naye Mangi mteule wa Machame Gilbert Shangali,
amewashukuru wananchi wa machame, kwa kuona anafaa na hivyo kumpa heshima hiyo,
ambayo inamfanya kuwa mmoja wa viongozi wa kimila katika himaya hiyo.
Chifu mteule Gilbert Gilead Shangali ni mtoto
wa Kwanza kuzaliwa kwa Mangi (Gilead Abdiel Shangali) na ni Mjukuu wa Mwitori
Abdeil Shangali na ni Kitukuu cha Mangi Shangali Ndeserua.
Chifu mteule Gilbert Shangali, alizaliwa
Machame mwaka 1973,baadaye alijiunga na masomo ya shule ya msingi Machame
kuanzia mwaka 1980 hadi 1987. Shule ya sekondari (O-Level) Mwaka 1988
hadi 1992, na shule ya sekondari ya Siha (A-Level) mwaka 1993 hadi 1995.
Baada ya kumaliza masomo ya sekondari,
alijiunga na Chuo cha Oshwal Nairobi nchini Kenya, kuanzia mwaka 1996 hadi
1999. Ambapo alihitimu masomo yake na kuwa na Taaluma ya Uongozi na Utawala.
Mwenyekiti wa ukoo Dk. Harold Shangali wa kwanza (kushoto), Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi, Clement Andrea Shangali (katikati) na Katibu wa Umoja wa Machifu mkoa wa Kilimanjaro Joseph Mselle, wakiwa katika kikao cha maandalizi ya sherehe za kusimikwa mangi mkuu wa Machame Gilbert Shangali.
Machifu kutoka
mikoa mbalimbali Tanzania bara na Visiwani kushiri tukio la kusimikwa kwa Mangi
wa 52 wa Machame, tukio litakalofanyika kijiji cha Machame Wari , wilaya ya
Hai, mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa ukoo Dk. Harold Shangali
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya sherehe
za kusimikwa kwa Mangi mkuu wa Machame Gilbert Shangali. Clement Andrea
Shangali.


