CCM Kata ya Kaloleni yapendekeza Shule Mpya ya Sekondari iitwe Dk. Samia Suluhu

KALOLENI-MOSHI

Kamati ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Kaloleni, imependekeza Jina la Rais Samia Suluhu Hassani, liwe la shule mpya ya sekondari, inayojengwa katika Kata ya Kaloleni, iliyoko halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani humo.

Mapendekezo hayo yametolewa Desemba 12,2024 na Wajumbe wa Kamati hiyo, walipokuwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi inayotekelezwa ndani ya kata hiyo.

Akizungumza Mjumbe wa Kamati hiyo na Diwani wa Kata ya Kaloleni Nasibu Mariki, amesema Serikali Kuu, imeipatia Kata hiyo kiasi cha Sh milioni 584, kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari, kutokana na kuwepo kwa msongamano mkubwa wa wanafunzi katika shule ya Sekondari Msasani.

Mariki, amesema lengo la kujenga shule mpya ya sekondari ndani ya kata hiyo, limetokana na changamoto iliyowasilishwa, kwenye kikao cha Baraza la Maendeleo la Kata (WDC) kutokana na shule ya Sekondari Msasani, kuwa na idadi kubwa ya wananchi.

Amesema shule ya sekondari Msasani, ina takribani wanafunzi 1,400 wanaotoka kata ya Bondeni, Bomambuzi, Mabogini na Njoro, kuja kusoma katika shule hiyo.  

Aidha amesema serikali, imeleta fedha kiasi cha Sh milioni 140, shule ya sekondari Msasani, ambazo zilitumika kujenga vyumba vitano vya madarasa kwa Sh milioni 110, ujenzi wa  maabara Sh milioni 16 na ujenzi wa matundu saba ya vyoo kwa Sh milioni 14.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo Makamu mkuu wa shule ya Sekondari Msasani Godwin Momburi, kwa Kamati hiyo amesema  ujenzi wa shule mpya ya sekondari  ulianza Septemba 20 mwaka huu na kwamba kujengwa kwa shule hiyo,  itakwenda kupunguza msongamano wa wanafunzi waliopo katika shule ya Msasani.

Akihitimisha ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya (CCM), Kata ya Kaloleni Joshua Kojo, alisema kamati imeridhishwa utekelezaji wa mradi huo, kwani thamani ya fedha inaonekana pia na mradi huo, unatekelezwa kwa kiwango cha juu zaidi na hiyo, imeonesha ni jinsi gani Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inavyotekelezwa kwa kasi zaidi.

Sambamba na hilo Mwenyekiti huyo, amewataka mafundi wanaoendelea na ujenzi huo kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, ili ifikapo Januari 13, mwaka  2025 wanafunzi waweze kuingia madarasani.

Katibu wa CCM Kata ya Kaloleni Hamadi Mgonja na Mjumbe wa Kamati ya ujenzi Happiness Urio, wameishukuru serikali kwa namna inavyoleta fedha kwa ajili ya maendeleo ndani ya kata hiyo, jambo ambalo,  limewapunguzia mzigo wazazi wa kuchangia fedha tofauti na huku nyuma ambapo kila mzazi litakiwa kuchangia.

Naye Afisa mtendaji Kata ya Kaloleni Iliyasa Mnjejah, alimshukuru Diwani Mariki kwa kujenga hoja na kufanikisha kupata fedha za kujenga shule hiyo mpya, huku akiwaomba wananchi kuhakikisha mradi huo wanautunza ikiwemo vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi huo.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kaloleni Joshua Odhiambo Kojo (katikati), Mjumbe wa Kamati na Diwani wa Kata ya Kaloleni Nasib Mariki wa Kwanza kushoto na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kaloleni, ambaye pia ni Mjumbe katika Kamati hiyo Ndama wa Ndama.





Moja ya Vyumba vya Madarasa shule ya  Sekondari Mpya yanayojengwa kata ya Kaloleni.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Msasani , Mwl. Godwin Marick Momburi, wa pili      (kushoto), akitoa maeleo ya ujenzi kwa Wajumbe wa Kamati ya CCM Kata ya Kaloleni, walipotembelea ujenzi wa shule mpya ya Sekondari
Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kaloleni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, wakikagua Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari inayojengwa katika Kata hiyo. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.