MOSHI-KILIMANJARO
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Bi. Mwajuma Nasombe, amefanya uamuzi wa kumuondoa kazini mtumishi mmoja wa idara ya sheria, aliyeonekana kuathirika na ulevi kazini.
Hayo yamo kwenye hotuba yake, wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa hiyo, desemba 13, 2024,ambapo amesema kwamba mtumishi huyo alikuwa akionyesha tabia ya kuingia kazini akiwa amelewa, licha ya kuonywa mara kadhaa kuhusu tabia hiyo.
Mwl. Nsombe, ameongeza kuwa wako baadhi ya watumishi wengine pia wamekuwa wakifika kazini wakiwa wamelewa, jambo linalodhalilisha utumishi wa umma na kuwaonya kuacha tabia hiyo.
Amesema “Huwezi ukawa mtumishi wa umma, ukawa unakunywa pombe kupita kiasi, mpaka unabebwa kupelekwa nyumbani, hii ni aibu kubwa, lakini pia unadhalilisha utumishi wa umma, mtumishi wa umma lazima hata maisha yako unapokuwa nje ya kazi, ni lazima ujitambue kuwa wewe ni mtumishi wa umma,”amesisitiza Nasombe.
Aidha Mkurugenzi huyo, amepiga marufuku kwa mtumishi yeyote wa umma, kufika kazini akiwa amelewa au kutumia vilevi wakati wa kazi, na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini.
Mwl. Nasombe, ameyataja matumizi ya vilevi kazini kama mojawapo ya mifano ya utovu wa nidhamu, huku akisema kuwa ni aibu kwa mtumishi wa umma ambaye anadhihirisha tabia za kulewa, huku akieleza kuwa nidhamu ni nguzo muhimu ya mafanikio katika utendaji kazi.
“Nidhamu, inahusisha pia kuheshimu taratibu, viongozi, na wenzao kazini, uzembe, tabia mbaya, na uvunjifu wa maadili ni baadhi ya mifano ya utovu wa nidhamu, ambayo inaweza kusababisha kuvunjwa kwa kanuni za kudumu za utumishi wa umma za mwaka 2009.”amesema.
Katika hatua nyingine
Mkurugenzi huyo, amewataka watumishi wa halmashauri ya Manispaa hiyo, kufanya
kazi kwa kushirikiana na kusaidiana ili kazi katika idara ziweze kufanyika kwa
ufanisi.
Akizungumzia suala la uwajibikaji
Nasombe , amesema ni moyo wa utendaji bora, ambapo kila kila mmoja ana jukumu
la kuhakikisha anatimiza majukumu yake kwa uaminifu na weledi.
“Serikali ilianzisha mfumo
wa upimaji, utendaji kazi kwa watumishi na upimaji wa taasisi (PEPMIS) ambayo
sasa inajulikana kama mfumo wa e-Utendaji, ili kila mtumishi aweze kuingiza
mipango yake ya kazi na kisha kutoa taarifa za utendaji wa kazi hizo kwenye
mfumo, kulingana na mpango ambao kila mtumishi ameingia.
Ameongeza kuwa “Jambo la kusikitisha ni kwamba amepokea orodha ya watumishi ishirini na nane (28) ambao hadi sasa hawajaingiza mpango wao wa kaazi katika mfumo huo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, watumishi hao wameshindwa kuwajibika kwa kutotii maelekezo ya serikali na wanastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuvunja kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022 kanuni 42 (8) ikisomwa pamoja na kanuni za kudumu za utumishi wa umma za mwaka 2009.













