"Joseph Tadayo Achaguliwa Kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Kilimanjaro"

MOSHI-KILIMANJARO.

Wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Kilimanjaro, wamefanya uchaguzi wa kumchagua Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Joseph Anania Tadayo, kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara mkoani humo, ambaye pia ndie Mkuu wa mkoa huo Nurdin Babu, alimtangaza Wakili Tadayo, kuwa ndie Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, baada ya wajumbe wa kikao hicho kumchagua kushika wadhifa huo.

"Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wajumbe wa Bodi kwa kuitumia vizuri demokrasi yenu na kuweza kumchagua Wakili Msomi Joseph Tadayo kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi hii…hongereni sana," amesema Babu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho  cha kwanza cha Bodi ya Barabara kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa mkoa huo, Babu amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mkoa huo umetengewa jumla ya Sh bilioni 73.103 kati ya fedha hizo Sh bilioni 49.186 zitatekeleza miradi iliyo chini ya TARURA ikihusisha matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 1,266.56

Aidha amesema Sh bilioni 23.917 zimepangwa kutumika katika miradi mbalimbali ya matengenezo na ukarabati wa barabara zilizopo chini ya TANROADS ikihusisha Sh bilioni 14.049 kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara huku kiasi cha Sh bilioni 9.168 kutoka Mfuko wa Maendeleo kwa ajili ya ukarabati wa barabara.

Babu amesema Sh bilioni 1.921 zitatumika kwa  ajili ya uendeshaji na usimamizi wa ofisi, Sh milioni 145.231 kwa ajili ya uendeshaji wa mfumo wa usimamizi na matengenezo ya barabara na madaraja, usimamizi wa hifadhi ya barabara na usalama wa barabara.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa, ameagiza Wakala wa barabara TANROADS na TARURA kuhakikisha kwamba, wanafanya usanifu wa miradi yote, kikamilifu na kuandaa mikataba vizuri ambayo masharti maalum yaendane na vifungu  vya mkataba mama (General Conditions of Contract).

“Tumekutana hapa kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo na changamoto zinazo ikabili sekta ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na ujenzi na matengenezo ya madaraja katika mkoa wetu,”amesema Babu.

Kwa upande wake Mbunge Tadayo, aliwashukuru Wajumbe hao, kwa kumchagua kuwa Makamu mwenyekiti wa Bodi hiyo na kuahidi kuwapa ushirikiano ili kuweza kfanikisha katika sekta hiyo ya miundombinu ya Barabara mkoani humo.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.