MWANGA-KILIMANJARO.
Serikali mkoa wa
Kilimanjaro, imewataka Wananchi mkoa huo, kuchangamkia fursa za kiuchumi
zinazotokana na sekta ya utalii zilizopo katika maeneo yao kwa kufanya biashara
mbalimbali ili kuendeleza uchumi wao na wa mkoa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa jana na
Katibu Tawala mkoa huo, Kiseo Nzowa,
katika hafla ya uzinduzi wa Tamasha la Mwanga na Mbio za Mwanga Marathon zilizofanyika
desemba 27,2024 Wilayani humo katika
viwanja vya CM Msuya.
Nzowa alisisitiza
umuhimu wa utalii katika kukuza ajira na biashara na kuwahimiza wananchi wa
wilaya hiyo, kutafuta njia za kuunganishwa na sekta hiyo ili wawezae kunufaika
na fursa zilizopo.
Aidha aliutaka uongozi wa
Wilaya hiyo kuhakikisha kwamba wanavitangaza vivutio vya utalii vilivyopo ili
kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza ndani ya wilaya hiyo
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Mnkunda, ameitaka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuharakisha ujenzi wa barabara ya Karamba ndea, kuelekea lango la hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na hivyo kukuza utalii na mapato ya halmashauri kwa ujumla
Aidha alisema serikali
wilayani humo, imejipanga, kuhakikisha kwamba maeneo yote yenye vivutio vya
utalii wanakwenda kuyalinda ili kuchochea Uchumi, pamoja na kuwakaribisha
wawelezaji wa ndani, kuja kuwekeza katika sekta ya utalii.
Munkunda alisema Wilaya
hiyo ina malengo ya kuanzisha kituo kidogo cha forodha, kupitia lango hilo, ili
kusaidia watalii wanaotoka hifadhi ya Taifa Tsavo nchini Kenya, waweze kupata
huduma za kiforodha ndani ya lango hilo.
Kwa upande wake Mbunge wa
Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, alisema toka serikali ya awamu ya sita kuingia
madarakani, imerudisha ule mfumo wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekya
ya umma, jambo ambalo limewezesha kuweko kwa maendeleo makubwa ndani ya wilaya
hiyo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Seleman Mfinanga na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Japhari Kubecha, ambao ni wazaliwa wa wilaya hiyo, walimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Munkunda, kwa kuja na wazo la kuanzisha mbio hizo ambazo zimewakutanisha Wanadiaspora na kuweza kukaa kwa pamoja na kuweza kufahamiana.