Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro Seleman Mfinanga, akionesha medali yake mara baada ya kumaliza mbio za Km 10.
MWANGA-KILIMANJARO.
Hatimaye Mwanga
Marathon & Festival 2024 imefanyika kwa mara ya kwanza katika viunga vya Wilaya
ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, ambako kumeshuhudiwa watu mbalimbali wakiwamo
viongozi wa Siasa wakishiriki mbio hizo zilizowakutanisha zaidi ya watu 500.
Miongoni mwa Wanasiasa
walioshiriki mbio hizo ni pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro Seleman Mfinanga, ambapo alisema mbio za marathon
zina faida ya kiafya, ajira na uchumi.
Akizungumza na Waandishi wa habari, baada ya kumaliza mbio za Kilometa 10; Mfinanga alitoa shukrani zake za dhati kwa Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bi. Mwanahamis Munkunda, kwa kuthubutu kuanzisha wazo hilo la kila mwishoni mwa mwaka.
“Tamasha hili linakwenda kuibua na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya wilaya ya Mwanga pamoja na kuchochea fursa za kiuchumi.”alisema Mfinanga.
Mfinanga aliongeza kuwa Mwanga Marathon & Festival kwa ushirikiano na Kisangara Tours litaifungua Wilaya ya Mwanga kiuchumi na kiutalii.
Kwa upande wake Bi. Munkunda alisema, Tamasha ambalo ni la Msimu wa Kwanza kufanyika Wilayani humo, litatumika kama njia kuwafungulia milango ya fursa katika sekta ya utalii ambayo kwa sasa inaitangaza nchi vizuri pamoja na kutoa ajira kwa wingi.
“Wilaya ya Mwanga imejaliwa kuwa na vivutio vingi ya kihistoria na mandhari nzuri, ambazo ni fursa kwa wana Mwanga, niwaombe wananchi kuvitumia fursa hizi, kwa ajili ya kuongeza kipato na kuifungua Wilaya yetu.”alisema DC Munkunda.
Wengine walioshiriki
mbio hizo ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Lameck Michael
Mlacha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Karia Rajabu Magaro,
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga Mwl. Ibrahim Mnzava, Mbunge wa Jimbo
la Mwanga Wakili Joseph Anania Tadayo, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga
Mwanahamisi Munkunda, Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mwl. Raymond Mwangwala, Mkuu wa
Wilaya ya Tanga Japhari Kubecha na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) Simon Maigwa.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga Japhari Kubecha (kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro Seleman Mfinanga, wakijipongeza mara baada ya kumaliza mbio za km 10 zilizoandaliwa na Uongozi wa Wilaya ya Mwanga.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro Seleman Mfinanga, akiwa katika picha ya pamoja na wakimbiaji wengine walioshiriki mbio za Mwanga Marathon-2024 zilizofanyika uwanja wa CD Msuya.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro Seleman Mfinanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Japhari Kubecha, Emmanuel Msemo Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Paul Bina Katibu wa UVCCM Wilaya ya Mwanga, na Mwenyekiti wa UWT Moshi Mjini, Teddy Komba.