MWANGA-KILIMANJARO
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro
Nurdin Babu, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Mbio za Mwanga Festival and
Marathon-2024 zitakazofanyika desemba 27, mwaka huu Wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa
habari desemba 26,2024, kuhusu hali ya maandalizi ya mbio hizo, Mkuu wa Wilaya
ya Mwanga Mwanahamisi Mnkunda, amesema Mkuu wa Mkoa amekubali mwaliko wa kuwa
Mgeni Rasmi wa mbio hizo zinazolenga kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo
wilayani Mwanga.
DC Mnkunda, amesema Babu ndiye
atakayeanzisha mbio hizo ambazo zitaanzia uwanja wa CD Msuya, huku
akiwataka wananchi wa Mwanga, kuzipokea
mbio hizo kama dirisha la kiuchumi na kujiandaa kuendena na ongezeko la
mahitaji ya kijamii.
Amesema mbio za Mwanga
Festival and Marathon, zinatarajia kuwaleta pamoja watu zaidi ya 1,000, ambao watahitaji chakula, malazi, mavazi, usafiri,
na aina nyinginezo za burudani, huku akitoa shime kuchangamkia fursa hiyo.
“Mwanga Festival and
Marathon, tunatarajia kuwaleta watu zaidi ya 1,000, ambao watahitaji chakula, malazi, mavazi, usafiri,
na aina nyinginezo za burudani, shime tuitumie fursa hii kujipanga vilivyo,
Wilaya ya Mwanga ina mengi ya kutoa;
tuchangamkie fursa hiyo,” amesema DC Mnkunda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mwanga Festival and Marathon Frida Mberesero, amesema jumla ya wanariadha 500 kutoka Wilayani humo, wanatarajia kushiriki mbio hizo, zijulikanazo kama za Mwanga Festival and Marathon Season One 2024 zitakazofanyika Desemba 27, mwaka huu.
Amesema maandalizi ya mbio hizo, yamefikia asilimia 100 ambapo wanaridha 500 watashiriki mbio hizo, zikiwa na lengo la kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.
“Huu ni msimu wetu wa kwanza wa mbio hizi za Mwanga Festival and Marathon, tunashukuru wananchi wa Mwanga wamehamasika kwa wingi kushiriki mbio hizi,”amesemaMberesero.
Amesema mbio hizo zitakuwa za kilometa 5 na Km 10 ambazo zitaanzia uwanja wa CD Msuya majira ya saa kumi na mbili kamili alfajiri, ambapo pia zitashirikisha vijana, watoto na wazee, huku Kauli Mbiu ya mbio hizo ni “Kuvumbua na Kuboresha Vivutio vya Asili Vilivyopo Wilaya ya Mwanga.”
Akizungumza mmoja wa washiriki wa mbio hizo, Rajabu Mshana, ambaye amejiandikisha kukimbia
mbio za Km 10 amesema ameshawishika kukimbia mbio hizo, baada ya kuvutiwa na nia
ya waandaaji hao, waliokuja na wazo la kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo
wilayani humo.









