SIHA-KILIMANJARO
Zaidi ya wakulima 300 Wilayani
Siha mkoani Kilimanjaro, wajiunga na mfumo
wa ruzuku ili waweze kunufaika na mbolea na mbegu bora zinazotolewa kwa bei ya
ruzuku.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti
wa mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini Gothard Liampawe, ameyasema hayo Desemba 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari, Wilayani humo, ambapo amesema kwamba ili mkulima aweze kunufaika na ruzuku za mbolea zitakazotolewa
msimu 2024/2025 wa kilimo ni lazima awe amesajiwa kwenye ofisi yake ya kijiji.
Liampawe, amesema baada ya wakulima
kujisajili katika vitabu, taarifa hizo zitaingizwa kwenye mfumo wa kidigitali
utakaoonesha idadi ya wakulima na mahitaji ya mbolea kwa kila mkulima, kulingana
na taarifa walizojaza kwenye fomu hizo na hivyo kurahisisha upatikanaji wa
bidhaa hiyo kwa wakati.
“Serikali inatekeleza mpango wa ruzuku kwa wakulima ambao wanapaswa kujisajili, sisi kama TFRA tuliamua kuja kuweka kambi hapa wilaya ya Siha, ili kupitia mbio za Siha Marathon, ili tuweze kuwasajili wakulima maana tunatambua kuna wakimbiaji na wakimbiaji hawa ndio wakulima wetu,”amesema.
Aidha amesema kupitia mbio
hizo, wakulima wapya, walikuwa hawajajisajili na wakulima wengine walikuja
kuhuisha taarifa zao, kwani usajili huo ni kuwatambua wakulima halisi kupitia
viongozi wa vijiji yalipo mashamba yao na hivyo kuwa na taarifa sahihi za
mkulima ikiwa ni pamoja na majina yake, ukubwa wa shamba na mazao anayolima.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa halmashauri ya Siha Dk. Haji Mnasi, ametoa shukrani kwa ujio wa viongozi
kutoka TFRA na kukiri kuwa ujio wao umesaidia kuongeza uelewa zaidi kwa wakulima wa namna sahihi
ya utekelezaji wa agizo hilo.
“Nichukue fursa hii,
kuishukuru serikali kwa namna ambavyo, imeendelea kutoa elimu juu ya uelewa wa
pamoja katika kufanikisha upatikanaji wa mbolea ya ruzuku.”amesema Dk. Mnasi. 






