Tadayo; Aishukuru Serikali kwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma

Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro wa kwanza kushoto, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Munkunda katikati na Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, wakishiriki mbio za kujifurahisha za km 5 Fun Run km.

MWANGA-KILIMANJARO

Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mkoani Kilimanjaro Wakili Joseph Tadayo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kuimarisha ushirikiano wa serikali na sekta binafsi, jambo ambalo limewezesha kuongeza wigo wa ajira kwa vijana nchini.

Tadayo aliyasema hayo Desemba 27,2024, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya hiyo, waliokuwa wamejitokeza kushiriki uzinduzi wa Tamasha la Kwanza la Mwanga Marathon, lililofanyika katika viwanja vya CD Msuya Wilayani humo na kuwakutanisha wakimbiaji zaidi ya 500.

“Katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tangu awe Madarakani, tumeshuhudia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025, ambapo kazi za maendeleo zimerudisha ule mfumo uliokuwepo awali wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya Umma.”alisema Wakili Tadayo.

Alisema tangu Rais Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani, jimbo la Mwanga limeweza kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo ambayo huko nyuma haikuwepo.

Alisema kuna hospitali kubwa ya Profesa Ngoma, imejengwa Kata ya Kwakoa, ambayo inatoa matibabu ya Kibingwa, lakini pia ziko hoteli  kubwa zilizojengwa na watu binafsi ndani ya Wilaya hiyo, ikiwemo hoteli ya KKKT Lodge, Mwanga Star Lodge, Dongodo hotel na kwamba matokeo hayo yote ya ni utendaji kazi mzuri wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Alisema uwepo wa mshikamano kati ya sekta binafsi na umma, umepelekea kufanikisha kuanzishwa kwa Tamasha la Kwanza la Mwanga Marathon, jambo ambalo lilikuwa lifanyike kama tamasha la kifamilia tu, lakini kwa sababu ya uhusiano mzuri kati ya sekta binafsi na Umma, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Munkunda, aliweza kuwaunganisha wadau wa maendeleo na kufanikiwa jambo hilo kuwa la Kiwilaya.

Tadayo, aliyataja mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha mabasi ya kwenda na kutoka mikoani, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kisangara kinachotoa Shahada ya Maendeleo ya Jamii, ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA, ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya, ujenzi wa jengo la Utawala, ujenzi wa barabara ya lami ya By Pass ya CD Msuya.

Pia alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya, imeipatia Wilaya ya Mwanga gari jipya la kubeba wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya hospitali mpya ya Wilaya, pamoja na fedha nyingine kwa ajili ya  ujenzi wa barabara ya lami ya Maliasili na CRDB zilizopo ndani ya Wilaya hiyo.

Akizungumzia mkakati wa sekta ya Utalii, Mbunge huyo, alisema Serikali inakwenda kulifungua lango la Karamba Ndea ili kukuza utalii na kuongeza mapato ya halmashauri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga Mwl. Ibrahim Mnzava, alimshukuru mkuu wa Wilaya Mwanahamisi Munkunda, kwa kuwaunganisha wana Mwanga lakini pia na kufanikisha kuibuliwa kwa vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya Wilaya ambavyo vilikuwa havitambuliki.

Mkurugenzi wa Mashindano ya Mbio za Mwanga Marathon and Festival Nelson Mrashani kushoto, akimvisha Medali Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, baada ya kumaliza mbio za kujifurahisha za Km 5.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.