MWANGA-KILIMANJARO
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga
Mwanahamisi Munkunda, ameitaka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani
humo, kuharakisha ujenzi wa barabara ya Karamba ndea, inayoelekea kwenye lango
la hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, jambo ambalo litakuza utalii na mapato ya
halmashauri kwa ujumla.
Munkunda, aliyasema hayo Desemba
27,2024, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Tamasha la michezo lijulikanalo
kama (Mwanga Marathon and Festival 2024), lililofanyika katika viwanja vya CM
Msuya.
Alisema kufunguliwa kwa
lango hilo, litakwenda kukuza utalii na kuongeza mapato ya mtu mmoja mmoja,
halmashauri na taifa kwa ujumla.
Aidha alisema Wilaya hiyo
pia ina lengo la kuanzisha forodha ndogo kupitia lango hilo, ili kusaidia
watalii wanaotoka hifadhi ya Taifa Tsavo nchini Kenya ili waweze, kupata huduma
za kiforodha ndani ya lango hilo.
“Ninamshukuru na kumpongeza
sana Mkurugenzi wa Kisangara Tours Frida Mberesero, kwa kazi kubwa ambayo
ameifanya ya kuviibua na kuvionesha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo
wilaya hapa, ambavyo tutavitumia kama sehemu ya kuchochea utalii ndani
yetu,”alisema DC Mnkunda.
Alisema kama Wilaya pia wamejipanga,
kuhakikisha kwamba maeneo yote ya utalii wanakwenda kuyalinda ili kuchochea
uchumi pamoja na kuwakaribisha wawelezaji wa ndani, kuja kuwekeza kwenye sekta
ya utalii.
Kwa upande wake Katibu
Tawala mkoa mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Nzowa, aliutaka uongozi wa wilaya hiyo
kuhakikisha kwamba wanavitangaza vivutio vya utalii vilivyopo ili kuvutia
wawekezaji wengi kuja kuwekeza ndani ya wilaya hiyo.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, alisema mkakati wa serikali ni kwenda
kulifungua lango la Karamba Ndea ili
kukuza sekta ya Utalii, na kuongeza
mapato ya halmashauri.