Viongozi wa kimila mkoani Kilimanjaro wamshukuru Rais Samia

HAI-KILIMANJARO

Viongozi wa kimila mkoani Kilimanjaro (Machifu), wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza utamaduni, mila na desturi za Watanzania, ambapo wamekuwa akiwapa kipaumbele katika shughuli za kiserikali kupitia ushirikishwaji wa viongozi wa mila ambao ulionekana kushuka kwa kipindi kirefu.

Hayo yamo kwenye hotuba yake Mwenyekiti Mstaafu wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT), Frank Marealle, wakati akitoa salamu za pongezi kwa Mangi mkuu wa Machame, Gilbert Gilead Shangali, aliyesimikwa kuwa Mangi wa himaya hiyo, hafla iliyofanyika viwanja vya Isareni, kijiji cha Wari, Wilaya ya Hai, mkoani humo.

“Kwa niaba ya machifu wa mkoa wa Kilimanjaro, ninaomba kumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameamua kuupa kipaumbele utamaduni wetu wa Watanzania, kupitia mikutano mbalimbali ya machifu na ushirikishwaji wa viongozi wa mila na desturi katika shughuli mbalimbali za kiserikali,”amesema Chifu Marealle.

Amesema anachokifanya Rais Samia ni kuhakikisha jamii za Kitanzania hazipotezi utamaduni wake na zinautumia utamaduni huo katika kuhamasisha amani, mshikamano maelewano na maendeleo endelevu ya nchi.

“Kwa miaka mingi mila na tamaduni za kitanzania zilionekana kutokuthaminiwa, lakini Rais Samia  ametambua umuhimu wake na kufufua umuhimu wa tamaduni zetu, tunamshukuru sana Chifu Hangaya (Rais Samia Suluhu Hassan) yeye kama kiongozi namba moja wa Machifu wote Tanzania, ameona umuhimu wa kuenzi mila na tamaduuni zetu ambazo zilikuwa zimeachwa kupewa kipaumbele, kutoka na uongozi wake madhuubuti, ameufufua na kuupa thamani mkubwa utamaduni wetu wa Mtanzania,”amesema Chifu Marealle.

Aidha amesema amani, umoja na mshikamano tulionao Watanzania ni wa kulindwa sana kwa sababu kuna baadhi ya mataifa mengine yanatamani kuwa na amani iliyoko kwetu lakini wanashindwa kupata tunu hiyo.

“Rais Samia amekuwa mfano wa kuigwa, katika kuhakikisha jamii za Watanzania, zinahifadhi na kutunza utamaduni wao, ambao unachochea amani, mshikamano, maelewano, na maendeleo endelevu, huku akikumbusha kauli ya Mwalimu Julius Nyerere aliyosema kwamba “Taifa lisilo na utamaduni wake ni kama kundi la watu waliojikusanya bila mwelekeo”, amesema.

Katika hotuba yake Chifu Marealle, alimtaka Mangi wa Machame kushirikiana na Serikali na jamii kwa ujumla katika kutatua migogoro isiyohitajika na kuhakikisha amani na mshikamano vinaendelea kutamalaki ndani ya jamii.

“Nichukue fursa hii kuasa utumie nafsi yako kuhamasihsa utunzaji wa mazingira ambayo yana umhimu mkubwa kwa maisha ya wanadamu”, amesema.

Aidha ametoa rai kwa Mangi huyo kuhakikisha anashirikiana na wananchi katika shuhghuli za kimaendeleo ambazo zitaboresha maisha ya watu ili wawe raia wema na wenye afya njema kutokana na ukweli kuwa uimara wa Taifa unatokana na watu wenye afya njema.

Akitoa neno la shukrani Mangi Gilbert Gilead Shangali, ameahidi kushirikiana na Serikali kuanzia ngazi zote na kuwa kiungo muhimu katika kushughulika na masuala yote yanayohusu majukumu yanayohitaji nafasi yake kama kiongozi wa kitamaduni, yakiwemo ya utunzaji wa mazingira, kuendeleza mila na desturi zilizo nzuri, malezi na makuzi ya watoto na jamii kwa ujumla.

Aidha amesema atahakikisha anashirikiana na serikali,  kushughulikia na kuhakikisha masuala ya ukatili kwa watoto, akina mama na wazee yanakomeshwa ili kuwa na jamii yenye upendo, umoja na mshikamano.

Nae Mshiri kutoka Wilaya ya Rombo George Kavishe, amesema kitendo cha Rais Samia kutambua mchango wa viongozi wa kimila ni jambo jema na anapaswa kupongezwa na kuungwa mkono na kila mmoja ili kutimiza azma yake ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kulinda na kudumisha tamaduni na maadili mema kwa jamii.

Akizungumza Mangi kutoka jamii ya Ki-maasai Wilaya ya Same Paulo Kiboko ole Munga, amesema viongozi wa kimila ni kiungo muhimu kati ya wananchi na serikali.

“Viongozi wa Kimila (Machifu), hushirikiana na serikali kuanzia ngazi zote katika kutatua migogoro ili kutokuipa serikali mzigo mkubwa katika kushughulikia changamoto ambazo zingeweza kutatuliwa na viongozi wa kimila”, amesema.


 






 








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.