MACHAME-KILIMANJARO
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Askofu Fredrick Shoo, alisema viongozi wa kimila wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanasimamia mila, desturi na tamaduni zilizo nzuri katika jamii.
Akofu Shoo, aliyasema hayo jana, wakati wa hafla ya kusimikwa kwa Mangi wa Machame Gilbert Gilead Shangali, ambapo alimshauri kiongozi huyo wa kimila kuwa mwenye maono, anayesimamia mila na desturi njema pamoja na kuongoza kwa kufuata maadili mema.
“Ninakupongeza kwa kutawazwa kwako, kwa tendo hili umefanywa kuwa kiongozi mkuu wa kimila kwa wananchi wa Machame, wewe ni alama na utambulisho wa taratibu mila na desturi za wamachame,”alisema Askofu Shoo.
Amesema “Nipende kukutakia Baraka za mwenyezi Mungu, kwamba mila zilizo nzuri, desturi zilizo nzuri, za wamachame, ukazisimamie na wewe mwenyewe ukawe mwenye maono na hizo mila, tamaduni na desturi zilizo nzuri,”alisisitiza.
Amesema Mangi wa Machame Shangali Ndeserua, ndie alikuwa wa kwanza kuwapokea wamisionali waliofika Machame,kuja kwetu hapa ni kutokana na kutambua mchango wa Mangi Shangali, katika kuleta nuru ya injili, pia alikuwa na hofu ya Mungu, hivyo nakuomba na wewe ukaige mfano huo.
Aidha Askofu Shoo, amemshauri kiongozi huyo wa kimila kuhakikisha kwamba suala la utunzaji wa mazingira analihimiza kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii.
Kwa upande wake Sheikh wa mkoa wa Kilimanjaro Shaban Mlewa, alisema kiongozi akiwa ni mtu mwenye tamaa, atawafanya hata wananchi wake, anaowaongoza kuwa na tamaa na kumsihi mangi Gilbert kutojiingiza huko.
.jpg)

















