MOSHI-KILIMANJARO.
Mamlaka ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), imepanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh
bilioni 10 kwa mwaka 2024/2025 lengo likiwa ni kuimarisha upatikanaji wa huduma
za maji kwa wananchi wanaowahudumia.
Mkurugenzi mtendaji wa
(MUWSA) Mhandisi Kija Limbe, ameyasema hayo desemba 17, 2024 wakati akitoa
taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2024/2025 kwenye Kikao cha Kamati ya
Ushauri ya Mkoa (RCC), na kusema kuwa Mamlaka hiyo imeweka vipaumbele
ambavyo vitazingatiwa katika mpango huo, ili kufikia lengo la upatikanaji wa
huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wote.
Amesema MUWSA imepanga
kukusanya na kutumia jumla ya Sh bilioni 10, kati ya fedha hizo Sh
bilioni 3.5 ni fedha kutoka Serikali Kuu, Sh bilioni 1, mkopo
kutoka Mfuko wa Taifa wa Maji, Sh bilioni 1.2, fedha za ufadhili kutoka KFW
huku Sh bilioni 4.2 kutoka kwenye Mapato ya ndani ya Mamlaka kwa ajili ya
uwekezaji.
Amesema, kupitia
mapato yake ya ndani Mamlaka hiyo, pia imefanikiwa kusimamia na kukamilisha
utekelezaji wa mradi mpya wa Majisafi na ujenzi wa chanzo cha Karanga Darajani,
ambapo wananchi wa kata za Pasua, Bomambuzi, na Mabogini, wameanza kunufaika na
huduma ya upatikanaji wa Majisafi na salama.
Mhandisi Limbe, amesema
kwa kutumia mapato ya ndani, Mamlaka hiyo imefanikiwa kuongeza mtandao mpya wa
usambazaji wa Majisafi kwa kilomita 104.395, kuongeza mtandao wa majitaka
kilomita 7.4 pamoja na kufanya ukarabati wa mtandao chakavu kwa zaidi ya
kilomita 23.21, kuunga jumla ya wateja wapya 4,308 kwenye huduma ya Majisafi
huku wateja wapya 47 wameungwa kwenye mtandao wa majitaka.
Vilevile amesema
Mamlaka hiyo, imefanikiwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa mwezi,
kutoa wastani wa Sh bilioni 1.1 hadi kufikia makusanyo kwa mwezi wastabni wa Sh
bilioni 1.3
Mbunge wa viti maalum
mkoa wa Kilimanjaro Shally Raymond, alimpongeza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji
Moshi Kija Limbe, kwa jitihada kubwa anazozifanya za kuhakikisha upatikanaji wa
huduma ya majisafi na salama kwa wananchi zinapatikana kwa muda wote.
Naye Katibu wa Mbunge
wa Jimbo la Vunjo Gulatone Masiga, ametoa ushauri kwa Mamalaka ya Maji MUWSA
kuendelea, kutoa elimu kwa umma kuhusiana na matumizi sahihi ya maji na namna
bora ya kutunza na kulinda miundombinu ya maji kwa huduma endelevu sambamba na
kutafuta vyanzo vya maji mbadala ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji.
Kwa upande wake Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amemuagiza mkugugenzi wa Mamlaka ya Maji
(MUWSA), kuanza kutekeleza ufungaji wa Pre-paid meter (Mita ya Malipo ya kabla)
kwa taasisi za umma kama ilivyo kwa LUKU kwenye (Umeme).







