RC Kilimanjaro; Amtaka Mangi Gilbert Gilead Shangali wa Machame kudumisha maadili

HAI-KILIMANJARO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amesema Serikali imedhamiria kuona Tanzania inakuwa na viongozi wa kimila, wanaoisaidia Serikali katika kutatua changamoto zilizoko kwenye jamii.

Aidha amesema viongozi wa kimila, wana msaada mkubwa katika kuelimisha na kufundisha juu ya kuongoza jamii, kuonya na kuwaadhibu wanaokwenda kinyume na maadili.

Akiwa mgeni rasmi katika tukio la kupandishwa daraja Mangi mkuu wa Machame Gilbert Gilead Shangali, Babu amesema,  mkoa wa Kilimanjaro uko mstari wa mbele kulinda na kudumisha mila na desturi za kiafrika.

"Mimi sitakasirika, wala sitashangaa kama mkichukua hatua kwa mujibu wa taratibu zenu za kimila, matarajio yetu kama Serikali ya mkoa ni kuhakikisha nidhamu iliyopotea inarejeshwa,"amesema RC Babu.

Amesema kwa sasa Tanzania, imeingioa katika wimbi kubwa la vitendo vya ulawiti na ushoga, huku akitoa rai kwa Watanzania na wana Kilimanjaro kwa ujumla, kutokupenda kujiingiza kwenye  mambo ambayo hawakuzaliwa nayo, kuiga utamaduni wa nchi za magharibi kutawaharibu watoto."

"Jamii imekumbwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili, maendeleo ya Teknolojia hasa katika upande wa mawasiliano, yamesababisha athari na kumuomba Mangi Gilbert Gilead Shangali, kuhakikisha anasimamia maadili ikiwa ni pamoja na vijana wanaolewa pombe nyakati za asubuhi wapewe adhabu kali,"amesema.

Naye Katibu Tawala mkoa huo Kiseo Nzowa, amempongeza Mangi Gilbert Gilead Shangali, kwa kutawazwa kuwa Mangi wa Machame.

"Nitoe pongezi zangu za dhati kabisa  kwa ndugu yetu Gilbert Gilead  Shangali, kwa kutawazwa kwako kuwa Mangi ,ukiwa kiongozi mwenzetu wa kijamii, sote ni viongozi wa kuwaongoza Wanannchi , tunakuahidi kama Serikali kukupa ushirikiano wa kila namna, utakaohitajika ili kuyafanya majukumu yao kuwa mepesi,"amesema Nzowa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Amani na Maridhiano Tanzania (JMT), mkoa huo, Askofu Jones Mola, amesema viongozi wa kimila wana mchango wa kipekee katika kujenga taifa lenye mshikamano, amani, utulivu na kuchangia katika maendeleo endelevu yanayozingatia urithi wa kitamaduni na maadili ya taifa.

Naye Sheikh wa mkoa wa Kilimanjaro Shaban Mlewa, amesema kiongozi akiwa ni mtu mwenye tamaa, atawafanya hata anaowaongoza kuwa na tama na kumsihi Mangi Gilbert Gilead Shangali kutokujiingiza na vitendo hivyo.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.