MOSHI-KILIMANJARO
Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania, Jones Mola, amewataka
wachungaji wanaoingizwa katika huduma ya Mungu, kuonyesha uaminifu na kujitolea
kwa dhati.
Hayo ameyasema Desemba 7, 2024, mjini Moshi, alipokuwa
akiongea na waandishi wa habari, akiwahimiza wachungaji kuwa na
uaminifu na moyo wa kujitolea katika kazi yao ya kumtumikia Mungu, huku akisema
kwamba watumishi wa Mungu wanapaswa kumwangalia Mungu kwanza na si watu, kwani
wengi hawakuwa na fursa ya kumwona lakini walichagua kumtumikia.
Akinukuu kitabu cha Injili ya Yohana 12: 26 Askofu Mola amesema
“Mtu ye yote anayetaka kunitumikia lazima anifuate; ili mtumishi wangu awepo
mahali nilipo; na mtu ye yote akinitumikia, Baba yangu atampa tuzo ya heshima.
Aidha Askofu Mola, amempongeza Shemasi Pauli Marki
Assey, anayetarajiwa kupandishwa daraja la uchungaji hivi karibuni, kwa kazi
hiyo ambayo Mungu amemuitia, atakiwa kutambua
kwamba Mungu ameacha watu wengi sana ambao hakuwaona na kumuona
yeye, ni vizuri akaenda kuonesha uaminifu na moyo wa kumpenda Mungu na
asiangalie watu bali amwangalie Mungu, amuongoze na roho mtakatifu kuitenda
kazi yake, alipende kanisa, nchi na viongozi wake.
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Africa Mission Evangelism
Church Tanzania Parokia ya Mamba (AMEC), ambaye pia ni Msaidizi wa Mkuu wa
Jimbo la Kilimanjaro Davis Makundi, amesema wanalo tukio la kiimani la
kumsimika, Shemasi Paulo Marki Assey kuwa mchungaji wa Kanisa
la AMEC Kata ya Kileo, tukio ambalo litafanyika Desemba 22 mwaka huu, kwenye
kata hiyo, Wilaya ya Mwanga, mkoani humo.
Mchungaji Makundi amesema tukio hilo, litatanguliwa na ibada ya
kawaida na baada ya hapo kutakuwa na tendo la kumsimika Assey kuwa mchungaji,
sambamba na tukio la kuwapokea wakristo watakaojiunga na kanisa la AMEC.
Amesema katika tukio hilo Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Mission
Evangelism Church Tanzania kutoka Makao Makuu Jijini Arusha, Baltazari Kaaya,
ndie atakaye msimika daraja la uchungaji, huku viongozi
mbalimbali wa kidini na kiserikali watakuwepo kushiriki ibada hiyo.
Aidha amesema kama kanisa wanauhitaji mkubwa wa watumishi wa Mungu
watakao hudumu katika shamba la Bwana, hivyo kusimikwa kwa mchungaji huo
atakwenda kuleta hamasa kubwa ya kuwahudumia wakristo wa kata ya Kileo
waliokuwa wamekosa huduma hiyo kwa kipindi kirefu.
Naye Shemasi Pauli Marki Assey, amesema tangu akiwa kijana mdogo, alikuwa
na wito wa kumtumikia Mungu, kwa hatua ambayo amefikia ya kusimika kwenda kuwa
mchungaji ni Mungu amesikia hitaji lake la Moyo wake la kwenda
kuihubiri injili kwa mataifa yote.
Viongozi watakaoshiriki tukio la kusimikwa mchungaji huyo mteule ni pamoja na Msaidizi wa Askofu Mchg. William Ayo, Mkuu wa Jimbo la Arusha Mchg. Elidaima Mushi, Katibu wa Theolojia Mchg. Yuda Pallangyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania Jones Mola, Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mchg. Willison Kawiche.
Pia viongozi wa Serikali walioalikwa ni pamoja na Mbunge wa Jimbo
la Mwanga Joseph Tadayo, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mwahamisi Munkunda, Mkuu wa
Polisi Wilaya ya Mwanga na Seikh wa Wilaya ya Mwanga, ambapo pia kutakuwepo na Kwaya
ya AMEC kutoka Msitu wa Tembo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, pamoja
na kwaya kutoka Jimbo la Arusha.





