MOSHI-KILIMANJARO
Kanali Deus Babuu, kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) amewashauri Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani, kuwahamasisha mabalozi wa nchi zao waje kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini jambo ambalo litakuza Diplomasia ya Uchumi, biashara, uwekezaji, utalii na tekbolojia nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza safari ya kupanda mlima mrefu Barani Afrika ulioko nchini Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro wenye urefu wa mita 5,895 sawa na futi 19,340, kwa lengo la kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, huku akisema kuwa kufanya hivyo itasaidia kukuza utalii na ushirikiano wa Kimataifa.
“Naomba kutoa ushauri wangu kwa Mabalozi wanaowakilisha Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani, kuwashawishi mabalozi wa nchi zingine wanakoziwakilisha waje kupanda mlima Kilimanjaro hii itasaidia kukuza diplomasia ya Uchumi, utalii na uwekezaji na hivyo kuongeza watalii wengi kuja kutembelea nchi ya Tanzania,”alisema.
Akizungumza Balozi wa Zambia Simon Sirro, alisema kuna umuhimu mkubwa wa Mabalozi wa nchi Wanachama wa SADC kuona umuhimu wa kuja kupanda mlima huo.
“Kazi yetu sisi Mabalozi ni kuvitangaza vivutio vya nchi yetu katika nchi tunazoziwakilisha, zikiwepo mbuga za wanyama, na mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kupata watalii wengi zaidi ambao watakuja na kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.”alisema Balozi Sirro.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mabalozi hao akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Brazil Adelardus Lubango, Balozi wa Tanzania nchini Burundi Gelasius Byakanwa na Balozi wa Kuwait Saidi Hussein Massoro, walisema zoezi la kupanda mlima Kilimanjaro katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, ili kuongeza idadi ya watalii wengi kutoka katika nchi wanazozisimamia.
Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayeshughulikia Sheria Ulinzi na Mkakati wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Ignas Gala, alisema Kampuni za utalii zilizopewa nafasi ya kuwafikisha wageni katika kilele cha mlima Kilimanjaro ikiwemo ZARA TOURS, African Senic,African Zoom Safari, pamoja na hifadhi ya TANAPA wamejipanga kuhakikisha wageni wote wanafika katika kilele cha mlima Kilimanjaro.
Kwa wake Mkuu wa msafara wa timu ya Mabalozi wa Tanzania Balozi Mahadhi Juma Maalim, aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa ya kuja kupanda mlima Kilimanjaro, ili kushirikiana na watanzania wengine kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru.
Mwakilishi kutoka Kampuni ya Zara Tours Bernard Sahini, amesema
ni Mara yetu ya 16 wakishiriki katika zoezi la kupandisha wageni mlima
Kilimanjaro, mara zote wamekuwa walikuwa wakiwapandisha maofisa wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWT) na ilipofika miaka 60 ya Uhuru walitanua wigo ili
kuwezesha taasisi nyingi zaidi kuweza kupata fursa ya kupandisha wageni, tangu
wameanzisha Kampeni ya Twenzetu Kileleni ni mara ya nne.




















