Mwanafunzi Rosemary Shirima, akimshukuru Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel, kwa namna alivyomsaidia katika matibabu yake na akaweza kufanyiwa upasuaji mkubwa wa tumbo hospitali ya Taifa Muhimbili.
SAME-KILIMANJARO.
Naibu Waziri wa Afya Dkt
Godwin Mollel amesema Wizara ya afya inaangalia uwezekano wa kushirikiana na Wizara
ya Tamisemi ili kuanza mchakato wa kutoa elimu ya afya mashuleni.
Dkt Mollel aliyasema hayo hivi
karibuni, wakati akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya tatu ya kidato cha nne
shule ya sekondari ya New Dawn, iliyoko
kata ya Njoro halmashauri ya wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema “Kwenye shule zetu,
ikiwemo shule ya New Dawn, kuna wanafunzi wanaotoka kwenye mazingira magumu,
mara nyingi, wengi wanakuwa wameathirika na mambo mengi yanayohusiana na
maswala ya kifamilia tangu utotoni”, amesema Dk. Mollel.
Amesema kutokana na hali hiyo baadhi ya wanafunzi wenye changamoto za namna hiyo huwa wanafanya maamuzi ambayo yanaonyesha wazi ya kuwa wameathirika kwa njia moja au nyingine na hivyo kupeleka tafsri ya moja kwa moja ya kuwa wanachangamoto za kiafya.
“Sisi kama Wizara ya afya
tunataka tuone namna ya kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, ili kushughulikia
maswala yanayohusiana na afya ya akili, kwenye shule ambazo zinadahili
wanafunzi kutoka sehemu mablimbali na wengi wao wakiwa ni wale wanaoishi katika
mazingira magumu”, amesema.
Ameongeza “Kama Rais Samia
Suluhu Hassan, alipozindua mpango wa lishe mashuleni, pia kwenye eneo la afya
kuna haja kuwa na mpango maalum unahusiana na maswala ya afya ya akili kwa
ksuhirikiana na taasisi za kiafya za wilaya na mikoa”, amesema na kuongeza,
afya nzuri ya akili ni msingi bora utakaowawezesha wanafunzi kufanya vyema
kwenye masomo yao.
Vilevile Dk. Mollel, akatoa rai kwa maofisa afya wa ngazi zote
kupita mashuleni kufanya utafiti, ambao matokeo yake yatakuwa msingi wa kuanza
kutoa elimu inayohusiana na afya ya akili mashuleni.
Aidha ameushukuru uongozi
wa shule ya New Dawn kwa kuanzisha shule hiyo, ambayo pamoja na mambo mengine
inatoa elimu ya sekondari kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na
yatima hadi kidato cha nne bila kuchangia gharama zozote.
“Uamuzi wa kuanzisha shule
hii umekuwa faraja si kwa wanafunzi tu bali na hata sisi ambao tulikuwa
tunachangia masomo ya baadhi ya wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu”,
amesema.
“Mimi mwenyewe nilikuwa
nachangia kati shilingi milioni 9 na milioni 10 kwa mwaka kwa ajili ya
kuchangia ghrama za masomo kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu, wanaotoka
katika Jimbo langu la Siha, lakini jukumu hili kwa sasa linashughulikiwa na
shule hii ya New Dawn”, amesema na kuongeza, kazi mnayofanya haina budi kuungwa
mkono.
Awali akizungumza Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la New Dawn Community
Dkt. Stephano Mshomi, amesema
uongozi wa shule umekuwa ukishirikina vizuri na idara za afya kuanzia zahanati
iliyopo kijiji cha Ishinde kwa kuwapa matibabu wanafunzi wenye changamoto za
kiafya.
“Tumekuwa tukipata
ushirikiano mkubwa kuanzia kwa wataalam wa afya walioko kwenye zahanati ya
kijiji, pamoja na hospitali ya wilaya ya Same, hospitali za rufaa ya Kanda ya Kaskazini
KCMC, na hospitali ya Taifa ya Muhimbili,”amesema Dk. Mshomi.
“Wanafunzi watatu
walifanyiwa upasuaji kati yao wawili walifanyiwa upasuaji wa kidole tumbo na
mmoja alifanyiwa upasuaji mkubwa wa tumbo mara tatu hospitali ya Muhimbili.
Wakitoa ushuhuda wao wa namna ambavyo uongozi wa shule
pamoja walivyo wasaidia kuokoa maisha yao Rosemary Shirima, na Nusra Mohamed,
hawakutarajia kama wangekuwa wako hai hadi leo hii.
“Nilikuwa na hali mbaya
sana, mimi mwenyewe sikutegemea kama ningekuwa hai hadi leo na kuweza kuhitimu
elimu yangu ya kidato cha nne,”amesema Rosemary.
