Dkt. Mollel: aahidi msaada wa Kompyuta 40, Mashine ya Photocopy shule ya Sekondari New Dawn


SAME-KILIMANJARO.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, ameahidi kuisaidia shule ya sekondari ya New Dawn, iliyoko Wilaya ya Same, kwa kutoa msaada wa Kompyuta 40 na mashine ya kudurufia (Photocopy), ili kuifanya shule hiyo kuendelea kuwa shule bora zaidi.

Dkt. Mollel, ameahidi kutoa msaada wa vifaa hivyo Novemba 30,2024, wakati wa hotuba yake ambayo aliitumia pia kujibu chanagamoto zilizotajwa katika risala iliyosomwa na mwakilishi wa wanafunzi, wakati wa hafla ya tatu ya kidato cha nne, ambapo pamoja na mambo mengine wamesema shule inakabiliwa na ukosefu wa kompyuta na mashine ya kurudufia (Photocopy), ukosefu wa uzio, maji safi na salama pamoja na maktaba.

Kuhusu suala la changamoto ya maji safi na salama shuleni hapo Dkt. Mollel  amesema atawasiliana na Waziri wa Maji Jumaa Aweso, ili aweze kuona tatizo lililopo katika shule hiyo ambayo inalea watoto hasa wanaotoka katika familia zenye vipato duni na yatima, waweze kusaidiwa kupata  maji karibu na eneo lao la shule.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la New Dawn Community  Internation Dkt.  Stephano Mshomi, amesema shule hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwahudumia wanafunzi wanaotoka katika familia zisizo na uwezo kutimiza ndoto zao.

Dkt. Mshomi, amesema taasisi ya New Dawn Community international ni daraja ambalo wanafunzi wataweza kupata elimu hadi kufikia ngazi ya vyuo na vyuo vikuu ili waweze kutimiza ndoto walizojiwekea.

Awali akizungumza Mkuu wa shule ya Sekondari ya New Dawn Emmanuel Kitadu, amesema shule hiyo, imekuwa ikifanya vizuri katika eneo la taaluma, kwani mpaka sasa shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 bora inayofanya vizuri katika Wilaya ya Same, mkoani humo.

Ameongeza kuwa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022 shule ilishika nafasi ya 10 kiwilaya  na mwaka 2023 shule hiyo ilishika nafasi ya 9 kati ya shule 57 zilizopo wilayani humo na kwamba kwenye eneo la michezo shule hiyo pia imekuwa ikishiriki vyema mashindano ya michezo mbalimbali ya kiwilaya, kimkoa na kitaifa.

Mwl. Kitadu, amesema kuwa licha ya kuwa na ufaulu mzuri, bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, maktaba na chumba cha kompyuta.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa kidato cha Nne, Rais wa Serikali ya wanafunzi Sebastian Christopher, amesema kwa miaka minne waliyokuwepo shule hapo, wamepata elimu bora ya darasani, iliyowajengea misingi bora ya kitaaluma ambayo itawawezesha kuendelea na elimu ya juu ili kutimiza ndoto zao.

Pia amesema wakiwa shuleni hapo, hawakuishia tu, kujifunza mambo ya kitaaluma darasani, bali walijifunza, kufanya shughuli mbalimbali za mikono ikiwemo kilimo, ufugaji na michezo, mambo ambayo amesema yatawasaidia kuepuka kwa wategemezi kwani wamejifunza kuwa wabunifu.

Shule ya New Dawn ilianza rasmi kidato cha kwanza mwaka 2019, ikiwa na jumla ya wanafunzi 36, ambapo shule hiyo, hutoa elimu kwa wanafunzi wa kike na kiume kwa kusimamia misingi ya nguzo kuu tano, ambazo ni makuzi ya kiroho, kitaaluma, kitabia, ujuzi na ufundi na huduma za kijamii.



















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.