MOSHI- KILIMANJARO.
Wizara ya Maliasili na Utalii, imesema itakiboresha kwa kukijenga upya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) na kwamba maboresho hayo yataimarisha uwezo wa chuo hicho katika kutoa elimu bora.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, aliyasema hayo Oktoba 01,2024 mjini Moshi akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya 27 ya chuo hicho, huku akisema kuwa chuo hicho kina umuhimu katika kukuza ujuzi na maarifa kwenye sekta ya misitu na utalii.
"Maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kukijenga upya chuo hicho, huku akitoa maagizo kwa Mkuu wa Chuo na Bodi yake , Mkurugenzi wa Mafunzo na mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, kukaa kwa pamoja na kutafuta mtaalamu atakayewatengenezea mchoro mzuri wa ramani ya chuo hicho,”amesema.
Akijibu risala iliyosomwa mbele yake na wahitimu hao Katibu (Mkuu) Maliasili na Utalii Dkt. Abbasi, amesema Wizara hiyo itanunua basi mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 65 kwa ajili ya wana chuo kwenda kujifunza kwa vitendo.
“Kwenye risala yenu mmesema mna uhaba wa usafiri kwa ajili ya kuwapeleka kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na mmesema gari mliyonayo ni ndogo mnakwenda mkiwa mmebanana na walimu….maelekezo yangu kwa TaFF nataka linunuliwe basi jipya lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 65, ndani ya mwaka huu wa fedha basi hilo liwe limefika katika chuo hiki.”amesema.
Aidha Katibu Mkuu huyo amemuahidi Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi FITI kumpatia gari, huku akimuomba radhi mkuu huyo kwa kutumia gari aina ya Pick up.
“Haiwezekani mkuu wa chuo akatumia Pick up, hii pick up utaangalia namna ya kuitumia, hatuwezi kuwa na mkuu wa chuo anayezalisha vijana kama ninyi, halafu anatumia pick up, kuanzia leo tunakupatia gari aina ya Land Cruzer Prado TXL yenye namba ya usajili STL 6702.”
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) Dkt. Tuli Msuya, amesema maombi ambayo FITI iliyaleta ofisini ya kuomba kujengewa hosteli, tayari Bodi ilishayapitisha na kabla ya mwezi wa 12 mwaka huu kazi ya ujenzi itaanzan rasmi.
Awali akizungumza Mkuu wa chuo Dkt. Zacharia Lupala, amesema chuo kinakabiliwa na uhaba wa hosteli ya watoto wa kike hali ambayo inawalazimu kulala nje ya chuo, na kwamba wana mpango wa kujenga hosteli yenye uwezo wa kulaza watoto wa kike 200 ambapo ujenzi huo utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.
“Tumeomba fedha kutoka kwenye Mfuko
wa Misitu Tanzania TaFF wakiridhia tutaanza kujenga mapema mwaka huu.”amesema
Dkt. Lupala.Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi-FITI Dkt. Zacharia Lupala, akisoma taarifa ya mahafali ya 27 ya chuo hicho mbele ya Katibu (Mkuu) Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi, akiwa katika picha ya pamoja na Wahifadhi wa Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro Chief Daudi Babu Mrindoko, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi Wakuu Wandamizi katika Sekta ya Wizara ya Maliasili na Utalii.