MOSHI-KILIMANJARO.
Wafanyakazi wa Kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Wilaya ya Moshi
mkoani Kilimanjaro, wametumia sehemu ya mishahara yao kufanikisha kununua gari la wagonjwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya
FT-Kilimanjaro Jaffari Ally, ameyasema hayo wakati wa kukabidhi gari hilo aina
ya Toyota Land Cruseir lenye thamani ya Sh milioni 219, ambalo limekabidhiwa katika
hospital ya TPC iliyopo chini ya usimamizi wa kiwanda hicho.
Alisema gari hilo litakuwa
likitoa huduma za afya kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa
miaka mitano.
Amesema lengo la kuanzishwa
kwa mradi wa Mama Bus ni kutokana na kuwepo kwa changamoto ya usafiri kwa makundi
hayo, waliokuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilometa 20 kutafuta huduma za
matibabu.
Hatua hiyo inatajwa kuwepo
na vifo vingi vya mama wajawazito na watoto iliyotokana na kutokuwepo kwa
huduma za afya karibu.
“Mradi wa Mama Bus tulianza
na vijijiji vinne ambavyo ni Kiyungi, Kikavu, Mbuyuni na Utamaduni ndani ya
Arusha Chini na tumeongeza na kufikia vijiji tisa ambavyo ni Uhuru, Langaseni,
Mikocheni, Chemchem na Muungano ,ambapo Mama Bus hutembea kila siku kijiji
kimoja na kutoa huduma hizo.”amesema.
Ally aliongeza kuwa mradi
huo wa Mama Bus utawanufaisha wananchi wapatao 95,000 katika kata za Arusha
Chini iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na Kata ya Msitu wa tembo
iliyopo wilaya ya Simanjiiro mkoani Manyara.
Alisema kuwa kupatikana kwa
gari hilo kumechagizwa na mishahara ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ambao walikuwa wanakatwa mishahara yao kidogo kidogo
na kufanikisha ununuzi wa gari hilo.
“Kundi la akina mama
wajawazito na watoto ni makundi ambayo yanaambukizwa magonjwa ya mlipuko kwa
haraka hivyo FT-Kilimanjaro imefanya jitihada za kuokoa maisha ya makundi haya
kwa kuwasogezea karibu huduma za afya.”amesema Ally.
Kwa upande wake msimamizi
wa miradi ya FT-Kilimanjaro Lazaro Urio,
amesema awali walikuwa wakitoa huduma hiyo kwa kutumia gari aina ya Noah, ambayo
kwa sasa imechakaa kutokana na ubovu wa barabara hali ambayo ilikuwa
inahatarisha maisha ya mama wajawazito na watoto.
Amesema kuanzishwa kwa mradi huo kumesaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza vifo vya mama na mtoto
kwa maeneo ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro na upande wa Simanjiro mkoani Manyara.
“Tumekuwa tukitoa huduma za
afya kwa kutumia gari aina ya Noah kwa zaidi ya miaka 10, kwa kipindi cha masika
gari hii ilikuwa haiwezi kwenda kutokana na uchakavu wa barabara, tunawashukuru
wadau wa maendeleo waliojitokeza kununua
gari hili wakiwemo kampuni ya mafuta PUMA, Toyota, TPC na FEMI.”amesema.