Waandishi waendesha ofisi mkoani Kilimanjaro (TAPSEA) wametakiwa kuzingatia usiri, uadilifu na kuwa na lugha njema wanapopokea wageni kwenye ofisi wanazohudumia ili kuendelea kujenga mahusiano mema katika ya ofisi hizo na wanaofuata huduma katika ofisi hizo.
Ushauri huo umetolewa Novemba 9,2024 na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Nzowa, wakati wa hafla ya uzindzui wa chama cha makatibu waendesha ofisi (TAPSEA) kwa Mkoa wa Kilimanjaro, iliyopfanyika mjini Moshi, mkoani humo na kuhudhuriwa na waandishi waendesha ofisi zaidi ya 100 kutoka wilaya za mkoa huo.
Amewataka Waandishi waendesha ofisi hao kuhakikisha kwamba wanakuwa na uhifadhi mzuri wa nyaraka serikali, kuwa na lugha njema kwa wageni na udilifu ambayo ndio nguzo kubwa na nguzo muhimu katika huduma wanazotoa.
Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa amewataka Waandishi waendesha ofisi hao kuendelea kuzingatia uadilifu huku wakizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Ummai, sambamba na kuziheshimu katika muda wote, jambo ambalo amesema litawapa heshima zaidi katika kazi zao wanazozifanya.
Akiweka msisitizo katika usiri, Nzowa amesema utunzaji wa nyaraka ni muhimu kutokana na unyeti wa nyaraka za kiofisi, ambapo amesema kinyume cha hapo uvujaji wa nyaraka unaweza kuleta madhara makubwa kwa taasisi inayohusika na nyaraka hizo.
Katika hafla hiyo iliyokwenda sambamba na kuingizwa kazini viongozi wa TAPSEA mkoani Kilimanjaro, huku akiwakumbusha wanachama wa chama hicho kipya kuhakikisha wanajiendeleza kielimu ili kuzidisha ufanisi katika uekelezaji wa majukumu yao.
Aidha alitoa wito kwa mamlaka husika katika chama hicho kuhakikisha kuwa wanaume pia wanajiunga na chama hicho kwa vile wako ambao pia wanashika nyadhifa kama hiyo kwenye ofisi mbalimbali.
Akisoma risala kwa niaba ya Waandishi Waendesha ofisi Michael Sedekia amesema kuwa kuanzishwa kwa chama hicho ngazi ya Mkoa wa Kilimanjaro ni muendelezo wa chama hicho ambacho kilianzishwa katika ngazi ya kitaifa mwaka 2008.
Amesema kuwa malengo ya TAPSEA mkoani Kilimanjaro ni pamoja na kuwakumbusha wanachama wake kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, weledi, uwajibikaji, staha na heshima ili kuunga mkono juhudi za Mlezi wa TAPSEA Kitaifa ambaye Rais Samia Suluhu Hassan zinazolenga kuobresha maisha ya Watanzania.
Aidha Sedekia ameendelea kusema kuwa matarajio ya wanachama wa TAPSEA mkoani Kilimanjaro ni pamoja na kubadilishana mawazo, uzoefu katika kazi ili kuednana na teknolojia ya kisasa sambamba na kushirikiana katika shida na raha.
Akizungumzia changamto ambazo waandishi wamendesha ofisi ambazo wanakutana nazo na ambazo wanatarajia kuzifuatilia kupita umoja wao huo, ni pamoja na ile ya baadhi ya viongozi kutokuthamini waandishi waendesha ofisi ambapo amesema wakati mwingine hupewa majukumu yasiyoendana na ujuzi wao.
Changamoto zingine ni pamoja na waandishi waendesha ofisi kupewa majukumu nje ya majukumu yao na pia baadhi yao kunyima haki zao za msingi za kuhudhuria mkutano mkuu wa kitaaluma ambao hufanyika mara moja kwa mwaka.