Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro (DRBC) Sabas Salehe, akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Robo ya Kwanza ya mwaka 2024/2025, kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, mbele ya vyombo mbalimbali vya habari mkoani humo.
MOSHI-KILIMANJARO
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro, imezuia ununuzi wa majenereta mawili, uliokuwa
ufanyike kati ya Kampuni ya Uendelezaji na Uendeshaji wa kiwanja cha Ndege cha
Kilimanjaro (KADCO) na Kampuni ya uuzaji wa
majenereta ya African Power Machinery (APM).
Naibu Mkuu wa Takukuru mkoani humo Sabas
Salehe, ameyasema hayo Novemba 11, 2024, alipokuwa akitoa taarifa ya
utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha Robo ya Kwanza ya
mwaka 2024/2025, kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, mbele ya vyombo
mbalimbali vya habari mkoani humo.
Amesema Takukuru ilifanya ufuatiliaji wa kina, kuhusiana na miradi kutoka Kampuni ya KADCO ya ununuzi wa majenereta mawili yaliyokuwa yamefanyika kutoka Kampuni ya African Power Machinery kwa gharama ya Sh milioni 329.4, baada ya kuwasilishwa kwa jenereta hizo, zilibainika kuwa na mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na cable zilizokuwa zikitakiwa kununuliwa kuletwa tofauti na hizo.
Naibu Mkuu huyo wa Takukuru huyo, ameseongeza kuwa pia injini za jenereta hizo zilikuwa za zamani, huku baadhi ya maeneo ya jenereta hizo yalikuwa yana kutu na maeneo mengine yalikuwa yamepakwa rangi.
Amesema baada ya uchunguzi wao wa mchakato huo, walibaini kuweko kwa mianya ya rushwa na ubadhirifu, ambapo wal;iamua kuzuia fedha hizo zisilipwe na sasa wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini waliotaka kufanya ubadhirifu huo ili mkondo wa Sheria uchuke nafasi yake.
Katika hatua nyingine TAKUKURU mkoani humo,
imebaini kusuasua kwa ujenzi wa hospitali ya Manispaa ya Moshi kutokana na
Mkandarasi Humphrey Construction Co. Ltd kutokulipwa kwa wakati fedha zake.
Amesema baada ya ufuatiliaji wa mradi huo,
waliwasiliana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na kumshauri
mkurugenzi huyo kumlipa mkandarasi fedha anazodai kiasi cha Sh milioni 213.6
ili aweze kuendelea na ujenzi hospitali hiyo.
Akizungumzia suala la Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 27 mwaka huu Naibu Mkuu huyo wa
TAKUKURU mkoa wa Kilimanjaro, amewataka wakazi wa mkoa huo kuchagua viongozi waadilifu na wazalendo
watakaolinda na kutumia rasilimali za umma kwa maslahi mapana ya nchi na sio kwa maslahi yao binafsi kwani viongozi
wanaopatikana kwa njia za rushwa hutumia rasilimali za umma kurejesha fedha zao
walizohonga wakati wa uchaguzi.

