Jiwe la "Mkumbavana" jiwe ambalo watoto waliokuwa wakizaliwa na changamoto ya ulemavu, wazazi wao walikuwa wakiwapeleka na kuwatupa na kufia huko ili kuondoa laana na mikosi katika familia zao.
MWANGA-KILIMANJARO.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga
Joseph Anania Tadayo, anatarajia kutumia fursa ya kiutalii kupitia Tamasha la
Mwanga Festival and Marathon 2024, kutembelea vivutio vya utalii vilivyomo
katika jimbo hilo kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki tamasha hilo
litakalofanyika Desemba 27 mwaka huu.
Moja ya kivutio kikubwa ambacho
anatarajia kukitembelea Mbunge Tadayo ni pamoja na jiwe “Mkumbavana” jiwe ambalo
watoto waliokuwa wakizaliwa na changamoto ya ulemavu, wazazi wao walikuwa wakiwapeleka
na kuwatupa na kufia huko ili kuondoa laana na mikosi katika familia zao, na Wajerumani
walipokuja katika wilaya hiyo waliwaelimisha wananchi hao na kuacha tabia hiyo.
Akizungumza na Jukwaa la
Mwanga Festiva and Marathon Tadayo, amewakumbusha wananchi wa Mwanga kujenga
utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika wilaya hiyo, ikiwa
ni sehemu ya kukuza maarifa, ujuzi, afya ya akili na kuongeza pato la taifa.
“Wilaya ya Mwanga ni
miongoni mwa maeneo yaliyo na utajiri
mkubwa wa vivutio vya utalii ambavyo bado vinahitaji kutembelewa na
kutengenezewa simulizi zinazohitaji kuwafikia watu wengi zaidi ikiwemo ya mtunzi
asilia wa wimbo wa maarufu wa kizalendo wa Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa
moyo wote, ambaye anatoka wilaya ya Mwanga Kata ya Kifula.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Munkunda, amesema suala la uwekezaji kwenye
vivutio hivyo bado ni fursa nyingine iliyo wazi kwa watu walio na nia pasipo
kujali ni wazawa au wageni.
DC Munkunda anazitaja fursa
za uwekezaji zilizopo katika sekta ya utalii kuwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba
za kulala wageni, hoteli, kambi za watalii katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na Ziwa Jipe, huku akisema kuwa bado zipo fursa nyingi
za uwekezaji katika wilaya ya Mwanga na kinachohitajika ni maamuzi na uthubutu
wa wahitaji wenyewe.
Naye Mwenyekiti wa Kamati
ya maandalizi ya Mwanga Festival an Marathon Frida Mberesero, amesema kupitia tamasha
hilo wadau mbalimbali wameendelea kuhamasishwa kuja kutembelea vivutio vya
utalii vilivyopo wilayani humo.
Mratibu wa Tamasha hilo
Zawadi Mirambo, amesema Wilaya ya Mwanga kwa kushirikiana na wadu wa utalii
ikiwemo kampuni ya Utalii ya Kisangara Tours Ltd, wameandaa tamasha maalumu la
kukuza utalii, zikiwemo mbio kilometa 5, 10, na 21 huku Kauli mbiu ikiwa ni Mwanga Yetu, Utalii Wetu.
“Mbio hizi zitafanyika
Desemba 27 mwaka huu kuanzia saa kumi na mbili asubuhi, ambapo mbio za Km 5, hadi
barabara ya Lang’ata, mbio za Km 10 zikianzia uwanja wa Cleopa Msuya hadi
Standi ya reli Kisangiro huku mbio za Km 21 zikianzia uwanja wa Cleopa Msuya hadi
Kisangiro.
Ameongeza kuwa washiriki wa
mbio hizo watapata T-shert pamoja na medali na baada ya ya mbio hizo kutamatika,
itafuatiwa na Tamasha la Utalii litakalofanyika
katika ufukwe wa Nyumba ya Mungu, ambapo kutawakuwa na nyama choma, vyakula vya
asili, ngoma za Wapare na jamii ya
kifugaji ya Ki-maasai.
Amefafanua kuwa siku ya Desemba
28 mwaka huu kutakuwa na safari ya kwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi,
kwa wale watakoshiriki ziara hiyo watatakiwa kujiandikisha kwa kupitia namba ya simu ya 0755-002
886.
Amesema watu watakaopata fursa ya kutembelea hifadhi ya Mkomazi wataweza kuwaona Faru weusi, kwa ukaribu zaidi tofauti na hifadhi zingine ambazo unaweza kutembelea, Mbwa mwitu, Tembo, Twiga, Nyati na ndege wa aina tofauti.


