MWANGA-KILIMANJARO.
Jumla ya hekta 60 za misitu
zilizoko katika hifadhi ya misitu ya Kamwala One, Kindoroko, Kamwala two na
Mramba zilizoko Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, zimeteketea kwa moto kwa mwaka
huu, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo shughuli za kibinadamu.
Mhifadhi Daraja la Pili kutoka
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilayani humo Pius Clement Maganga,
ameyasema hayo Novemba 13,2024 wakati akizungumza na Waandishi wa habari
wilayani humo.
Amesema uharibifu
uliofanywa na mioto hiyo, uliathiri mpaka huduma za kijamii ikiwemo huduma za
maji, baada ya miundombinu ya usambazaji maji iliyokuwa inatoa maji ndani
ya misitu hiyo kuungua kwa moto na
kusababisha wananchi kukosa huduma hiyo.
“Kwa tathmini ya haraka tuliyoifanya
tukijumuisha misitu yote iliyoteketea mwaka huu, takribani hekta 60 ziliteketea
kwa moto”, amesema Maganga.
Ameendelea kusema kuwa changamoto
hiyo hutokea haswa nyakati za kiangazi ambapo wananchi wanapokuwa katika
kutayarisha mashamba yao kwa ajili ya shughuli za kilimo, ambapo huwasha moto
kwa ajili ya kuchoma majani yaliyoko shambani.
Amesema changamoto nyingine
ni ile ya wachungi kupeleka mifugo yao kwenye misitu kwa ajili ya malisho ya
mifugo yao kutokana na ukame wakati wa kiangazi.
“Hali hii imeleta athari
kubwa ikiwemo kwenye sekta ya utalii kutokana na misitu kuharibiwa vibaya; wito
wangu kwa wananchi waepuka tabia hizi za uharibifu ili misitu iwe salama na
hivyo kuchangia uchumi wa Taifa kupitia utalii wa ikolojia”, amesema.
Ameongeza kuwa “Ni vyema
watu wakajenga tabia ya kuwa na uzalendo na kuepuka shughuli ambazo zitaathiri
misitu kwa vile madhara hayatakuwa kwa misitu, wanyama na mimea tu bali hata
kwa wananchi wanaoishi kuzunguka misitu
hiyo”, amesema Maganga.
