MOSHI-KILIMANJARO
Taasisi za kielimu ikiwemo elimu ya ufundi, zimetakiwa kuanza michakato ya kupitia upya mitaala yao kabla ya wakati wake kuisha ili ihuishwe au itengenezwe mingine mipya kwa mujibu wa Sheria.
Wito huo umetolewa Novemba 13,2024 na Afisa Mdhibiti Ubora (taaluma) kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet) Dkt. Edward Mneda, wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo yanayohusiana na Kurejerea mitaala mipya ya ufundi, semina ambayo inafanyika katika Chuo cha Viwanda vya Misitu FITI Moshi, mkoani Kilimanjaro.
“Taasisi zinazoendesha mafunzo zinapaswa kuangalia muda wa kuisha kwa mitaala yao mapema ili mchakato wa (kurejerea) mitaala kuihuisha au kutengeneza uanze mapema; kwa mujibu sheria, ambapo shughuli hizo zinatakiwa kuanza miezi sita kabla ya mitaala hiyo haijaisha muda wake”, alisema Dkt. Mneda.
Alishauri kuwa ni vyema michakato hiyo iwe imekamilika ndani ya miezi mitatu kabla haijaisha ili iweze kuidhinishwa mapema na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
“Kama unavyofahamu kwamba Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ni baraza lililoanzishwa kisheria kwa sheria No. 129 kwa lengo la kusimamia Vyuo ambavyo vinatoa mafunzo katika sekta ya ufundi na ufundishaji, hivyo swala la kupitia upya mitaala hiyo ni la kisheria”, amesema.
Akizungumzia zoezi hilo Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu FITI Mohi Dkt. Zacharia Lupala, amesema kuwa zoezi hilo limewahusu wakufunzi wapya, walioajiriwa na serikali kwa ajili ya kutoa mafunzo katika chuo FITI ili waweze kupata utaalam unaohusiana na urejereshaji wa mitaala.
“Wakufunzi wapya pamoja na wahitimu wa chuo cha FITI wengi ni wageni kwenye kazi zao za ukufunzi, lakini wengi hawajawahi kushiriki zoezi hili la kuhuisha mitaala, hivyo wanatarajia kupata elimu inayohusiana na swala hilo kupitia mafunzo haya”, alisema Dkt. Lupala na kuongeza kuwa, kupitia mafunzo haya watapata mbinu za kuhuisha na utaratibu mzima wa kuandaa mitaala mipya.
Dkt. Lupaka aliongeza kuwa “Katika chuo chetu tuko katika zoezi la kurejea mitaala yetu ambayo iliandaliwa tangu mwaka 2019, zoezi hili ni kwa mujibu wa muongozo wa kisheria ambapo mitaala inatakiwa kurejerewa au kuhuishwa kila baada ya miaka mitano na kwamba mitaala ya chuo chetu iliyopo inatarajiwa kuisha muda wake ifikapo Mei mwaka 2025.



