Soko la Mbuyuni Manispaa ya Moshi kukamilika desemba 13,2024

MOSHI-KILIMANJARO

Kampuni ya Kitanzania ya Rock Tronic LTD ya mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro, inayojenga soko la kisasa la Mbuyuni katika Manispaa ya Moshi, inatarajia kukamilisha ujenzi huo ifikapo desemba 13, mwaka huu.

Hayo yamesemwa Novemba 13,2024 na Mhandisi wa Kampuni ya Rock Tronic Ltd Injinia Emmanuel Kisanga, wakati  akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo la mradi huo kwa ajili ya kujionea ujenzi wa soko hilo unavyoendelea.

Amesema mradi wa soko la kisasa la Mbuyuni, mpaka sasa umefikia asilimia 60 na kwamba ifikapo tarehe 13 mwezi desemba 13 mwaka huu soko hilo watalikabidhi na kuanza kutumika kutokana na kasi ya ujenzi inayoendelea.

Aidha Injinia Kisanga amewahakikishia wafanyabiashara wa soko la mbuyuni, kuanza kufanya biashara zao kwa muda uliokusudiwa kwani kazi zinazoendelea kwa sasa ni umiminaji wa zege, ambao umefikia asilimia 80, upauaji wa bati umefikia asilimia 20, ulazaji wa tofali umefikia asilimia 100 na ujenzi wa matundu ya vyoo umefikia asilimia 60.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadi ya wafanyabiashara wa soko hilo Zulfa Issa, Anitha Shirima, Anna Stewart pamoja na wananchi wenye makazi ya jirani na soko hilo, wameupongeza uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi  kwa kutimiza ahadi yao ya kuwajengea soko hilo, hatua ambyo inawapa matumaini wafanyabiashara wa soko hilo kurudi na kuendelea na biashara zao.

Setemba 24, mwaka huu Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro, iliyotembelea na kukagua ujenzi wa soko hilo ambapo Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mwajuma Nasombe, alisema soko hilo tayari limeanza kujengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.6 kupitia mapato yake ya ndani ambapo kiasi cha Sh milioni 800 zimekwisha kutolewa kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo na kati ya fedha hizo mkandarasi ameshalipwa Sh milioni 238.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, akisema kuwa Baraza la Madiwani kwa pamoja, walikubaliana kusimamisha miradi mingine yote iliyokuwa inatekelezwa kwenye kata zao ili soko hilo lijengwa kwa wakati.

Soko la Mbuyuni liliteketea kwa moto usiku wa februari 6 na kuacha wafanyabiashara zaidi ya 2,500 wakiwa hawajui la kufanya baada ya bidhaa zao zote kuteketea.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.