MOSHI-KILIMANJARO
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, imeipongeza Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuunga mkono maono na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuendeleza uzalishaji endelevu wa kahawa za hilo hali ambayo imeendelea kumnyanyua mkulima wa zao la kahawa na kuleta tija kwenye uchumi wa nchi kwa ujumla.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mariamu Ditopile Mzuzuri, ametoa pongezi hizo Novemba 15, 2024 kwa niaba ya Kamati hiyo, ilipotembelea na kukagua utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na TCB yenye makao makuu yake Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya kilimo hapa nchini.
“Dhamira ya Rais Samia ni kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo nchini, sote tunashuhudia namna ambavyo amewekeza kwenye kilimo, hivyo tunawategemea ninyi watendaji wake kuhakikisha, mnakwenda kuyatimiza yale maono ya rais ili kumsaidia mkulima mdogo ananyanyuka kiuchumi kupitia kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Primus Kimaryo, amesema dira ya Bodi hiyo ni katika kuhakikisha inakuwa kinara kwenye usimamizi na utoaji huduma Afrika, kwa kuweka mazingira wezeshi katika kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu.
Amesema TCB imejiwekea mpango mkakati wa miaka sita kuanzia mwaka 2020/21 hadi 2025/26 wenye vipaumbele vinne ambavyo ni kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa, kuwezesha upatikanaji wa bei shindani ya kahawa (competitive Price) na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwenye sekta ya kahawa.
Aidha amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 Bodi ya kahawa Tanzania (TCB) imezalisha miche bora ya kahawa milioni 22.6 ambayo ilisambazwa kwa wakulima.






