MOSHI-KILIMANJARO.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na mji wa Kerry ulioko nchini Ujerumani, zimeingia makubaliano na klabu ya mpira wa wavu (KVT) kukuza vipaji kwa vijana katika mchezo humo.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Shadrack Mhagama, ameyasema hayo Novemba 15,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini, baada ya kutembelewa na ugeni wa watu 15 kutoka nchini ujerumani, wakiwa wameongozana na mkufunzi wa mpira wa wavu barani afrika ambao wamekuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa wa wavu.
Amesema ugeni huo umeahidi kuboresha maeneo ya viwanja ikiwa sambamba na kujenga kituo cha mpira wa wavu kitakachokuwa na ofisi zake, ili kuendeleza mpira wa wavu katika halmashauri hiyo.
“Ugeni huu umekuja kutoa hamasa hapa nchini ili uweze kutupa motisha ya sisi kuendeleza mpira wa wavu katika halmashauri yetu ya Moshi, wamekuja na watatembelea maeneo mbalimbali ambayo wanaweza kuyaboresha na tukaendeleza mchezo huu, lakini pia watajenga na kituo cha mpira wa wavu,”.
Mkurugenzi huyo amemshukuru Rais wa shirikisho la mpira wa wavu duniani kwa kukubali kujenga miundombinu, kununua vifaa vya mchezo huo hali ambayo itakwenda kusaidia kunyanyua vipaji kwa vijana.
Amesema halmashauri ya hiyo inayo timu ya mpira wa wavu kutoka shule ya sekondari Old Moshi ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 iliibuka mshindi wa pili katika mchezo wa wavu katika ya halmashauri 100 nchini zilizoshriki mchezo huo.
“Halmashauri ya Moshi vijijini ina mahusiano na mji wa Kerry, nchini Ujerumani na hii inatupa fursa nzuri ya kuweza kuendeleza mchezo huu wa wavu, katika halmashauri yetu.”amesema Mhagama.
Kwa upande wake kocha wa mpira wa wavu nchini Alfred Selengia, amesema kuwa makubaliano hayo yatakwenda kukuza vipaji kwa vijana na hivyo kupata wachezaji wazuri wa mchezo huo wa wavu.
“Klabu ya mpira wa wavu ya KVT ya mji wa Kerry nchini Ujerumani, imeingia makubaliano na klabu ya mpira wa wavu ya Old Moshi, watapata nafasi ya kwenda nchini kujifunza mpira wa wavu na kuweza kuendeleza mpira huo.”amesema Selengia.
Ameongeza kuwa mpira wa wavu bado haujapewa kipaumbele kuanzia shule za msingi sekondari, kwani hakuna timu wala klabu inakwenda kutoa changamoto vijana wanaoishi kupata fursa hiyo
Nao baadhi ya wana michezo Nyakao Mwita na Sospeter Josephat, kutoka klabu ya mpira wa wavu shule ya sekondari Old Moshi, wamesema changamoto ya upungufu wa walimu, viwanja na vifaa vya vifaa vya michezo umesababisha mchezo huo kutokuchezwa na vijana wengi.
Mpira wa wavu ni mchezo ambapo timu mbili za wachezaji sita hujaribu kupata pointi kwa kuweka chini mpira kwenye kiwanja cha mchezo ya timu hiyo nyingine.


