Vyakula na vinywaji vya asili, kunogesha tamasha la utamaduni kilimanjaro

MOSHI-KILIMANJARO

Wananchi wametakiwa kuondokana na dhana ya kupenda kula vyakula kutoka nje ya nchi  na badala yake, wamesisitizwa kuzalisha na kula vyakula vya asili kama njia moja wapo sio tu ya kuimarisha lishe bali pia mfumo wa uzalishaji chakula.

Mwenyekiti wa Tamasha la Kilimanjaro Cultural Festival, Ansi Mmasi, ametoa wito huo, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, kuelekea tamasha hilo litakalofanyika Desemba 27 mwaka huu na kuwashirikisha takribani watu 2,000.

Mmasi amesema, vyakula vya asili vina virutubisho vyote na ni bora ukilinganisha na vyakula kutoka nje, kupitia tamasha la Kilimanjaro Cultural Festival (KCF) wameweka kipaumbele kwenye eneo la vyakula vya na vinywaji vya asili vya makabila yaliyoko mkoani humo,  kutokana na umuhimu wake.

“Vyakula hivi vya asili kwanza vina faida kubwa kiafya na kwenye lishe vyakula vya asili kama vile ndizi, mahindi, mboga za majani, na matunda yanayotoa virutubisho  muhimu vinavyosaidia katika kuimarisha afya ya jamii, kutokana na vyakula hivyo kutokuwa na kemikali .”amesema.

Amesema vyakula vya asili pia vinachangia ustawi wa kiuchumi  kwani uzalishaji wake unatoa fursa za ajira kwa wakulima na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi na hivyo kusaidia katika kuendeleza uchumi kwa mwananchi na taifa kwa ujumla.

Amesema faida nyingine amesema ni pamoja na kuhifadhi mazingira kwani kilimo cha malighafi zinazotoa au kutengeneza vyakula vya asili na vinywaji hutumia mbinu bora za kilimo endelevu ambazo zinalinda udongo na vyanzo vya maji na hivyo kusaidia kutunza mazingira.

Kuhusu vinywaji vya asili Mmasi amesema  vina faida za kiafya, ikiwemo chai za mtidawa ambayo husaidia katika kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza magonjwa mbalimbali.

Amesema mkoa wa Kilimanjaro vyakula na vinywaji vya asili vinaweza kuwa kivutio cha utali na kwamba kupitia  tamasha hilo wataihimiza jamii, serikali na wadau wengine kushirikiana katika kuhifadhi na kukuza vyakula vya na vinywaji vya asili kwa kuimarisha uzalishaji wa bidhaa hizo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wakichangia maendeleo ya kiuchumi, afya bora na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kilimanjaro Cultural Festival, Raymond Mushi, amesisitiza kuwa maendeleo ya nchi yanatokana na kuenzi utamaduni na mila za makabila, pamoja na vyakula vya asili ambavyo vimekuwa vikitumika kwa vizazi vingi, huku akisema kuwa  vyakula hivyo vilichangia katika maendeleo makubwa ya mkoa wa Kilimanjaro.

Naye mdau wa tamasha hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Biosafi, amesema kuwa tamasha hilo litatoa fursa kwa wafanyabiashara na wakulima wa mazao ya asili na kwamba  vyakula hivyo vitatangazwa na vitapatikana katika migahawa mbalimbali ya mkoa huo na hivyo kuongeza fursa za biashara na uchumi.




 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.