Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, waomba huduma mkoba (mobile-clinic) zianze kutolewa kwenye vituo vyao


MOSHI-KILIMANJARO.

Wadu wa elimu Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameiomba serikali kuanza kutoa huduma Mkoba (Mobile-Clinic), kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (day care center), ili watoto wenye mahitaji maalum waweze kutambuliwa mapema na kupata matibabu kwa wakati na hivyo kupunguza idadi ya watoto wenye ulemavu katika jamii.

Mkuu Chuo cha Mafunzo ya Montessori Ushirika wa Neema-Moshi, Mtawa Christine Nakey, ameyasema hayo Novemba 23,2024, wakati akitoa taarifa ya chuo kwa mgeni rasmi katika mahafali ya 32 ya wahitimu wa mafunzo ya ualimu na malezi ya watoto wadogo, kwa mfumo wa falsafa ya Dkt. Montessori, ambapo jumla ya wanafunzi 56 walihitimu elimu yao kwa ngazi ya cheti.

Mtawa Nakey, amesema  utolewaji wa huduma za Mkoba (Mobile-Clinc) itasaidia watoto wenye utapiamlo kutambulika mapema  na kupatiwa matibabu stahiki jambo ambalo litasaidia watoto hao kukamilishiwa chanjo.

Mkuu huyo wa chuo, ameiomba serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kulelea watoto wadogo mchana vinakuwa na walezi wenye taaluma inayohusiana na malezi na makuzi, pindi wanapotoa huduma hiyo waweze kutoa huduma iliyo bora na stahiki kwa watoto kwani kazi ya malezi inahitaji taaluma na sio bora malezi.

Aidha amesema chuo hicho, kimefanikiwa kuendesha semina ya malezi na makuzi iliyowahusisha wadau mbalimbali wakiwemo maafisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Moshi vijijini, ambapo pia wahitimu hao walifanikiwa kutembelea mahabusu ya watoto iliyoko manispaa ya moshi, kutembelea mbuga za wanyama, utengenezaji wa zana za kufundishia na kila mhitimu ameweza kupatiwa zana, zitakazomsaidia aendako kuzitumia ili kuibua vipaji mbalimbali vya watoto  pindi watakapovitumia. 

Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe halmashauri ya Moshi vijijini Dkt. Juma Mombokaleo,  ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amewataka wazazi kuwaendeleza zaidi kielimu watoto wao, huku akiwapongeza wahitimu wa mafunzo ya ualimu na malezi ya watoto wadogo kwa kuhitimu elimu kwa ngazi ya cheti.

Katika hatua nyingine Dkt. Mombokalea amevutiwa na vifaa pamoja na zana za kufundishia na kujifunzia vivyotumia na wakufunzi wa chuo hicho, hali ambayo inamrahisishia mwalimu ufundishaji wake na kuwafanya wanafunzi waelewe somo kiurahisi zaidi.

"Safari ya kumsomesha mtoto na kumuandaa kufanya vizuri ni ndefu sana, hivyo wazazi wanao wajibu wa kuendelea kushirikiana na walimu ili watoto waweze kujengwa kwenye misingi mizuri, kwani huo ndio uwekezaji wanaotakiwa kuufanya  wazazi kwa watoto wao ili waje kuwa kizazi kizuri kwa maendeleo yao binafsi, jamii inayo wazunguka na taifa kwa ujumla."amesema Dkt. Mombokaleo.

Naye Mwenyekiti wa wamiliki wa vituo vya malezi ya watoto wadogo mchana (Day Care Center) mkoa wa Kilimanjaro Osward Mlay, amesema kituo hicho, kinakabiliwa na changamoto ya walimu wenye taaluma ya malezi na makuzi ya watoto wadogo na kuwaomba wale ambao watakosa ajira,waweze kuwasiliana na kituo hicho ili kiweze kuwapatia ajira.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake Juliana Siwa, amekishururu Chuo cha Montessori Ushirika wa Neema-Moshi, kwa kuanza kutoa taaluma ya malezi ya watoto ngazi ya cheti, ambapo mafunzo hayo yanatolewa kwa njia ya vitendo yanayomsaidia kumwezesha mlezi kupata ustadi wa kumsaidia mtoto kuweza kujifunza kuwa na utaratibu, umakinifu na ubunifu pale anapotumia zana hizo katika kujifunza.

Chuo cha Mafunzo ya Montessori Ushirika wa Neema na Hellen Memorial ni mali ya Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na wanafunzi 14, ambapo kwa sasa chuo hicho kina uwezo wa kupokea idadi ya wanafunzi 92 kwa mwaka.

Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe Halmashauri ya Moshi Vijijini Dkt. Juma Mombokaleo,  ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Mahafali 32 ya wahitimu wa Mafunzo ya Ualimu na Malezi ya Watoto Wadogo, yanayotolewa kwa mfumo wa Falsafa ya Dr. Montessori Usharika wa Neema-Moshi.

Mkuu Chuo cha Mafunzo ya Montessori Ushirika wa Neema-Moshi, Mtawa Christine Nakey, akitoa taarifa ya Chuo kwa mgeni rasmi kwenye Mahafali ya 32 ya Wahitimu wa Mafunzo ya Ualimu na Malezi ya Watoto wadogo mchama (Day Care Center).

Mkuu Chuo cha Mafunzo ya Montessori Ushirika wa Neema-Moshi, Mtawa Christine Nakey.Mchg. wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Ushirika wa Daniel Anael Mlaki, ambaye pia ni Mlezi wa Ushirika wa Neema-Moshi.


Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vituo vya Malezi ya Watoto Wadogo Mchana (Day Care Center) Mkoa wa Kilimanjaro Osward Mlay.

Bi. Juliana Siwa, kisoma risala kwa niaba ya Wahitimu wenzake
Wanafunzi wa mwaka wa Kwanza Chuo cha Montessori Ushirika wa Neema Moshi


Mkuu Chuo cha Mafunzo ya Montessori Ushirika wa Neema-Moshi, Mtawa Christine Nakey, akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Ualimu na Malezi ya Watoto wadogo mchana ngazi ya cheti.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.