Best Simba: Serikali imejiimarisha kiuchumi kupitia miradi ya umeme

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro Best Simba, akizungumza na Walimu Makada Wazalendo, kuelekea Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 

ROMBO-KILIMANJARO.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro Best Simba, amesema serikali ya Awamu ya sita imefanya juhudi kubwa katika kuimarisha uchumi wa Tanzania kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ya umeme, ambayo imeongeza utosherevu wa Nishati hiyo nchini.

Simba aliyasema hayo jana katika Kijiji cha cha Ngaseni, kilichoko Wilayani Rombo mkoani humo, alipokuwa akizungumza na walimu makada wazalendo, katika kampeni zinazofanyika za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

"Serikali imefanya jitihada kubwa sana za kuhakikisha Tanzania inaendelea kujiimarisha kiuchumi, kwa kuanzisha miradi ya umeme, ambayo imeongeza utosherevu wa umeme nchini, lakini pia uwekezaji wa treni ya umeme, iliyoanza safari zake kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma."amesema Simba.

Katika mkutano huo Mjumbe huyo, alitumia fursa hiyo kuwataka Wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi Kwenda kuwapigia kura za ndio wagombea wanaotokana na CCM kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, utakaofanyika kesho kutwa Jumatano-Novemba 27 mwaka huu kwa  kuichagua CCM na kuipa ushindi wa heshima.

“Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuifanya Wilaya ya Rombo kuwa na maendeleo zaidi, ambapo wananchi wake watanufaika na Sekta ya  Utalii kupitia Filamu ya Royal Tour.

Simba amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Sh bilioni 62 zimeletwa na Serikali Kuu Wilayani humo, kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ambapo katika sekta ya Maji kiasi cha Sh bilioni 22 zimeletwa, Sekta ya  Elimu na Afya Sh bilioni 26 huku kiasi cha Sh bilioni 14 zikipelekwa kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA.

"Kwa sasa kila mwananchi anashuhudia namna miradi  ya maendeleo, ikitekelezwa wilayani Rombo, maendeleo yapo kila kona, ukienda ukanda wa tambarare Serikali inajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Holili-Tarakea hadi Nayemi, hivyo tunawaomba mkawachague viongozi wanaotokana na CCM ili waweze kuja kuendeleza miradi hiyo,"amesema Simba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilayani humo Anthony Tesha, amesema, Wilaya hiyo imejipanga kushinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa Wananchi wameona miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.

Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro, kimesimamisha wagombea katika vijiji vyote 159, Mitaa 60 na Vitongoji 2,257 vilivyoko katika mkoa huo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.