Manispaa ya Moshi yakabidhi vyombo vya moto vya usafiri vyenye thamani ya Sh milioni 84 kwa vikundi vya vijana

 

 

 

MOSHI-KILIMANJARO.

Halmashauri ya Manispaa  ya Moshi, imekabidhi pikipiki za matairi matatu tano na bodaboda  nane, vyenye thamani ya Sh milioni 84 kwa vikundi 14 vya vijana kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Akikabidhi vyombo ambavyo ni bodaboda  nane na bajaji tano, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amesema kuwa uwezeshwaji huo unatokana na fedha za makusanyo ya ndani, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutenga asilimia 10 kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.

“Rais Samia alielekeza fedha hizi ambazo wanapewa makundi haya, zitolewe bila riba ili kila mmoja awe mnufaika na kutumia fursa hii kumpongeza Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe, kwa kusimamia maelekezo hayo vizuri ambapo yamewezesha leo hii vijana kunufaika na mpango huu.”amesema RC Babu.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, amesema Manispaa  hiyo inatekeleza kwa vitendo  maelekeo yote ambayo yanatolewa na Serikali Kuu na kwamba inazingatia pia uwezeshwaji wa vijana katika sekta zote za uchumi na kijamii.

Mhandisi Kidumo, amesema fedha za kausha damu, zimekuwa ni kero kubwa sana kwa wajasiriamali hawa, huku akimshukuru Rais Samia kwa kukubalia kuirejesha tena mikopo hiyo isiyo kuwa na riba.

Naye Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo  Stuwart Nathael, amesema fedha hizo zitakwenda kuwa kwamua kiuchumi Wananchi hususani wakazi wa Manispaa ya Moshi, na kuwasisitiza kuhakikisha mikopo hiyo wanairejesha kwa wakati ili na wengine waweze kukopa.

Awali akizungumza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe, amesema jumla ya vikundi 65 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu  vimepatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 813.4.

Amesema kati ya vikundi hivyo vikundi 40 vya Wanawake  vilivyopata kiasi cha Sh milioni 468.1, Vijana vikundi 14 vimepata mkopo wa Sh milioni 319.6 na vikundi vya Watu wenye ulemavu 11 vimepata mkopo wa Sh milioni 25.7.

"Jumla ya vikundi 98 kutoka ngazi ya kata viliomba mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.1 ambapo vikundi vya Wanawake vilikuwa 59, Vijana 27 na Watu wenye ulemavu vikundi 12, viongozi wa  halmashauri  walikwenda kuvikagua na kuhakiki miradi ya vikundi vyote kwenye kata zote 21 na kubakiwa na idadi ya vikundi 65 vyenye sifa ya kupata mikopo yenye thamani ya Sh milioni 813.4,"amesema Mwl. Nasombe.

Aidha Nasombe amemshukuru Rais Samia  kwa kuirejesha mikopo hiyo ambayo inakwenda kuwanufaisha wananchi wengi wa Manispaa ya Moshi na hivyo kuwa na maisha bora.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.