Nurdin Babu: Awaongoza wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro kupiga kura Serikali za Mitaa

SHANTY-KILIMANJARO.

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu ameongoza wakazi wa Mkoa wa huo katika upigaji kura wa kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa, unaofanyika Novemba 27, 2024 nchini kote.

Majira ya saa mbili kamilia asubuhi  Mkuu huyo wa mkoa, alifika katika kituo alichojiandikishia cha kupiga kura cha Mtaa wa Makongoro, kilichoko Kata ya Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na kujiunga na foleni ya Wapiga kura ambapo zamu yake ilipofika alihakiki jina lake na kishwa kwenda kupiga kura yake.

Baada ya kupiga kura yake, Babu  alipata fursa ya kuongea  na waandishi wa habari, ambapo amesema, kuwa amefurahishwa na idadi ya wananchi waliojitokeza, kushiriki zoezi la upigaji kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku akiwataka kupiga kura kwa amani na utulivu na kisha kurudi majumbani mwao na kungojea matokeo.

“Kwa upande wangu nimefurahi kushirki zoezi hili ambalo ni haki yangu ya msingi na ni haki ya Watanzania wote Kikatiba; ni matumaini yangu wenzangu watajitokeza kwa wingi ili nao watimize haki yao hiyo”, amesema RC Babu.

Babu aliandamana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Kiseo Nzowa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji ambao pia ni wapiga kura wa mtaa huo.

Akizungumza baada ya kutekeleza zoezi hilo, Msimamizi wa Uchaguzi huo Mwl. Mwajuma Nasombe, amesema kuwa taratibu zote za uchaguzi zilikuwa zimekamilika na kwamba zoezi hilo lilianza saa mbili kamili za asubuhi kama ilivyokuwa imeelekezwa.

Mwl. Nasombe ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi, alipiga kura yake kwenye kituo cha Moshi Chapel kilichoko mtaa wa Kilimanjaro ulioko Kata ya Kilimanjaro Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, amewataka wananchi kurudi majumbani mwao baada ya kupiga kura na kungojea matokeo.

“Hakuna haja ya mtu kubaki kituoni baada ya kupiga kura kwa sababu yoyote, ikiwemo ile ya kudai kulinda kura; swala hilo liko mikononi mwa  Mawakala ambapo kila chama kilichoshiriki uchaguzi kina wakala ambaye ni mwakilishi wa chama husika”, amesema Msimamizi huyo wa uchaguzi Mwl. Nasombe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro Dkt Christopher Timbuka amesema kuwa zoezi hilo lilianza vizuri Wilayani humo na kwamba watu wamejitokeza kwa wingi kupiga kura hiyo, ambapo yeye alipiga kura kwenye kituo cha Wiri kilichoko kata ya Gararagua, Wilayani humo.

“Zoezi hili limeanza vizuri na inatia moyo kuona ya kuwa watu wengi wamejitokeza wakati wa awali kabisa baada ya vituo kufunguliwa; kinachotia moyo zaidi ni kuwa vijana wengi wamejitokeza tena mapema, hii ni ishara njema kuwa uhamasishaji wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu, umefanikiwa kwa kiasi kikubwa”, amesema Dkt. Timbuka.

Nae Mkuu wa wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni, ambaye alipiga kura yake kituo cha Stesheni, kata ya Stesheni Wilayani humo, amesema zoezi hilo limeanza vizuri na kwamba watu wamejitokeza kwa wingi na mapema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliojitokeza kushiriki upigaji wa kura, wameipongeza serikali kwa namna ambavyo imeweza kuliratibu zoezi hilo na kuwa jepesi kwao kuweza kupiga kura.

Mkazi wa Shanty town  Mhandisi Joachim Mahoo, amesema “Serikali za Mitaa zina umuhimu sana kwa maendeleo ya maeneo yetu tunayoishi, wito wangu wananchi  waliojiandikisha wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi huu,”.

Naye Mkazi wa Kata ya Kilimanjaro mtaa wa Makongoro Mwl. Emanuel Mushi amesema “Mwitikio wa wanannchi kushiriki zoezi la upigaji kura Serikali za Mitaa ni mzuri kwani hakutarajia kama wananchi wangeweza kijitokeza wingi huo.

Aidha maesema  uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndio mwanzo wa utawala kwani maendeleo yanaanzia kwenye mtaa wao, kama hutakuwa wamemchagua kiongozi ambaye ni mzuri maendeleo yataanzia kuharibikia katika eneo lao wanaloishi.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.