Nasombe: Wenyeviti Serikali za Mitaa mliochaguliwa, hakikisheni mnazingatia misingi ya Katiba ya nchi

MOSHI-KILIMANJARO.

Viongozi Serikali za Mitaa waliopata dhamana ya kuchaguliwa na wananchi katika maeneo yao, wametakiwa kwenda kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya katiba ya nchi.

Msimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe, ameyasema hayo Novemba 28,2024,wakati akizungumza na wenyeviti pamoja na wajumbe wa halmashari kuu ya mtaa, kabla ya zoezi la kuapishwa, lililofanyika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa wa kiliamnjaro.

Mwl. Nasombe amewataka viongozi waliopata dhamana ya kuaminiwa na wananchi, kwa kuwachagua, kuhakikisha kwamba wana kwenda kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali.

“Tambueni kwamba  ninyi mnawajibika moja kwa moja kwa wananchi, wasikilizeni na kutatua kero zao kwa wakati ili waendelee kuiamini Serikali iliyopo madarakani, kwani dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwatumikia wananchi, hivyo wale wote waliopewa dhamana ya kumsaidia rais, kila mmoja ahakikishe atimize wajibu wake ili wote tuwe tunaongea lugha moja ambayo ni kuwatumikia wananchi kwa kuwatatulia kero zao,” amesema Mwl. Nasombe.

Aidha amewataka viongozi hao, kujiepusha na urasimu usio na tija wakati wa kuwahudumia wananchi na kuhakikisha kuna kuwa na usimamizi mzuri wa fedha za miradi zinazotolewa na Serikali ili zitumike ipasavyo katika maeneo yao.

Nasombe ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, amewataka wenyeviti na wajumbe wa halmashauri kuu ya mtaa, kuzingatia utumishi bora wa umma unaoongozwa kwa misingi ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali na kwamba watumishi wote katika ofisi zao wafanye kazi kwa kushirikiana, kupendana, kuaminiana na kuepuka fitna na majungu kwa kuingiza masuala ya vyma, ukabila wala udini.

Maagizo mengine aliyoyatoa msimamizi huyo wa uchaguzi, amesema  wenyeviti hao pamoja na wajumbe wa kamati hizo, hawaruhusiwi kwenda kuanza mara baada ya kula kiapo hadi hapo watakapopata maelekezo kutoka kwa mamlaka husika.

“Ukiapishwa sasa hivi, huruhusiwa kwenda kuanza kazi, ninawaomba mtasubiri kwanza maelekezo ili muweze kuanza kazi, jukumu lililoko mbele yenu kwa sasa kwa kupata semina elekezi, ili mwenyekiti aweze kutambua majukumu yake na mjumbe wa mtaa anatakiwa kufanya nini,”nafahamu mna ari ya kwenda kuwatumikia wananchi, lakini nawaombeni kwanza muweze kuvuta subri hadi hapo tutakapotoa maelekezo na miongozo.”amesema Nasombe.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu hasa kwa kuzingatia mageuzi ya kidemokrasia yanayoendelea chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba mageuzi hayo yanalenga kuboresha uwazi na uaminifu katika mchakato wa uchaguzi.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.