Ruwasa Kilimanjaro yasaini mkataba wa ujenzi mradi wa maji Kihurio

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkoa wa Kilimanjaro Injinia Weransari Munisi wa kwanza kulia aliye vaa koti jeusi akisaini kandarasi ya ujenzi wa mradi wa maji kata ya kihurio wenye thamani ya Sh bilioni 4.1 wa tatu kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilida Mgeni akishuhudia utiaji wa saini hizo.

SAME-KILIMANJARO.

Wakala wa Maji  na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkoa wa Kilimanjaro, umesaini kandarasi ya ujenzi wa mradi wa maji katika kata ya Kihurio jimbo la Same Mashariki mkoani humo, na Kampuni ya   Fesam Construction Limited yenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam ambayo itatekeleza mradi huo kwa miaka miwili.

Meneja wa RUWASA mkoa wa Kilimanjaro Injinia Weransari Munisi, ameyasema hayo jana,  mara baada ya kusaini kandarasi hiyo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya same, na kampuni ya Fesam Construction Limited.

Amesema mradi ambao wananchi walikuwa wakiutumia ulijengwa kwa miaka ya 1970, ulijengwa wakati huo idadi ya watu walikuwa wachache, kwa sasa hivi idadi ya watu imeongezeka zaidi ya mara 10 hali ambayo ilikuwa ni changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji.

Injinia Munisi, amesema, ili kuondoa adha hiyo ya kuendelea kukarabati kila mwaka, serikali imeleta mradi mpya wa maji na kwamba kwa mwaka wa fedha 2024/2025  kiasi cha Sh Bilioni 4,178, 753, 349 zitakwenda kutumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi mpya wa maji.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa (RUWASA), Wilaya ya Same Injinia  Abdallah Gendaeka, amesema mradi huo utahudumia kata nzima ya Kihurio yenye vijiji vitatu vya Kakonkolo, Kongei na Uzambala vyenye wakazi 10,249 sawa na asilimia 3.9 ya wakazi waishio vijijini.

Amesema mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili kuanzia tarehe desemba 2024 hadi desemba 2026 na kwamba utahusisha ujenzi wa miundombinu mipya, ikiwemo ujenzi wa dakio la maji kutoka mto Sesemi, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 54.9 , ujenzi wa tangi kubwa lenye lita 500,000, vituo 51 vya kuchotea maji na vivunja nguvu (presha) pamoja na ukarabati wa matangi yaliyopo.

Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni, amemtaka mkandarasi huyo kujenga mradi huo kwa kuzingatia ubora unaotakiwa, sanjari na kuzingatia muda wa kukamilisha mradi huo ili wananchi waanze kupata huduma ya maji hususan katika maeneo ya kutolea huduma za kijamii.

Aidha mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi wa Kihurio kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa mkandarasi kwenye kipindi chote cha utekelezaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na kuwa walinzi wa kwanza wa mitambo itakayotumiwa na wakandarasi kutekeleza mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo,  mkazi wa Kihurio Aza Sadick Mashambo, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mradi huo ambao utakwenda kuwaondolea adha ya maji ambayo walikuwa wakiipata kwa kioindi kirefu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Kampuni ya Fesam Construction Limited Injinia Charles Maganga, ameahidi kuifanya kazi hiyo kwa wakati kulingana na mkataba unavyomtaka ili mradi huo, uweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Kata ya Kihurio ina jumla ya wakazi 10,249, imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama hali inayowalazimu wakazi hao kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Kilimanjaro Injinia Weransari Munisi, Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilida Mgeni na Mkurugenzi wa Kampuni ya  Fesam Construction Limited Injinia Charles Maganga, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa utekelezaji wa  mradi maji Kihurio.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.