Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji, akikabidhi mfano wa hundi ya Sh milioni 141.8 kwa baadhi ya wana kikundi waliopata mkopo huo, baada ya serikali kurejesha mikopo hiyo kwa makundi maalum.
MOSHI-KILIMANJARO.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, imetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 141.8 kwa vikundi 10 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa serikali wa 2024/25.
Hayo yameelezwa Novemba 20,2024 na Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo Stella Magor, wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo hiyo, iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, ulioko Moshi, mkoani humo.
“Mikopo hii itakayokabidhiwa leo ni kuanzia Julai, 2024 hadi Septemba, 2024, ambapo Sh milioni 74,182,000 itatolewa kwa vikundi 6 vya wanawake na jumla ya Sh milioni 67,500,000 itakabidhiwa kwa vikundi vinne vya vijana”, amesema.
Amesema, “Mikopo hii ni utekelezaji wa Sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa sura namba 290 na Kanuni zake za mwaka 2024 za utoaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu”, amesema Magori.
Kuhusu wana vikundi hao, Stella amesema kuwa wamepatiwa mafunzo mbalimbali ili kuongeza tija katika miradi wanayoitekeleza.
“Mafunzo waliyoyapata ni pamoja na yale yanayohusiana na utatuzi wa migogoro, usimamizi wa biashara na matumizi sahihi ya raslimali za umma ili kudhibiti mianya ya rushwa.”
Ameendelea kusema kuwa wanufaika wa mikopo hiyo watapata fursa ya kuboresha biashara zao zikiwemo zile za kilimo, ufugaji, biashara aina mbalimbali, ufugaji na shughuli za kuongeza tahamni ya mazao mbalimbali.
Ameelezea matumaini ya halmashauri hiyo kuwa wanufaika wa mikopo hiyo wataitumia vyema ili kuimaisha uchumi wao binafsi na ule wa wilaya kwa ujumla huku akitoa rai kwa waliokopa fedha hizo kuwa watarudisha mikopo waliyochukua kwa wakati, ili inufaishe na wengine na pia kuifanya kuwa endelevu.
Akikabidhi mikopo hiyo Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji ametoa wito kwa waliokopa mikopo hiyo kuitumia kama inavyotarajiwa.
“Nitoe rai pia kwa mamlaka husika kuhakikisha elimu pia inatolea kwa watu wenye ulemavu ili nao waweze kunufaika na mikopo hiyo maana kwenye hafla hii nimeona wanawake na vijana tu, ndiyo waliopata mikopo hii”, amesema Kaji.
Kwa upande wao, Wabunge waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua upya mikopo hiyo ambayo wamesema ni fursa itakayowawezesha wananchi kujiendeleza kiuchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wabunge hao wamewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyowekwa na pia wairudishe kwa wakati.
Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo Ema Massawe, Mary Mongi, Stella Mtei na Jackson Mringa, wameishukuru serikali kwa kuirejesha mikopo hiyo kwani itakwenda kuwanufaisha na kuahidi kuirejesha kwa wakati, huku wakisema kuwa
serikali ilipositisha mikopo hiyo waliyumba kiuchumi.