Manispaa ya Moshi kuvitumia vikundi vya Vicoba utoaji elimu ya chanjo

MOSHI-KILIMANJARO

Uongozi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, umesema kuwa uko tayari kuongeza nguvu ya utoaji wa elimu ya afya kuhusu Chanjo kupitia vikundi vya huduma ndogo za fedha vya Kijamii (VICOBA) vilivyopo ndani ya Manispaa hiyo.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro Injinia Zuber Abdallah Kidumo, ameonesha kufurahishwa na namna mafunzo hayo yanavyoshirikisha jamii moja kwa moja kwa kutumia ubunifu.

Injinia Kidumo, amesema ameridhia kuyapokea mawazo yaliyotokana na mafunzo hasa kwa kuwatumia akina mama waliko kwenye vikundi vya kiuchumi vya VIKOBA na kuja na mkakati wa mifumo itakayo saidia vituo vya kutolea huduma za afya kusomana ili kurahisisha uratibu wa huduma za chanjo.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku nne ya kuijengea uelewa kwa jamii umuhimu wa kuimarisha huduma za chanjo (HCD), yaliyofanyika mjini Moshi mkoani humo Injini Kidumo, aliwapongeze Wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kwa kuja na ubunifu huo wa kushirikisha jamii moja kwa moja kuanzia hatua za mwanzo hadi mlaji wa mwisho.

"Niwaahidi kwa kuwatumia akina mama hawa katika vikundi vya kukopa (VIKOBA), tutaifikia jamii kwa wingi zaidi na kinachotakiwa tu kwa sasa ni kuhakikisha tunashirikiana katika kuhakikisha tunakuwa na mfumo unaoweza kusomana kutoka kituo kimoja cha huduma za afya hadi kingine,”amesema Injinia Kidumo.

Akizungumza Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, amesema zaidi ya mikakati 300, imependekezwa ikiwemo kuyatumia majukwaa ya akina mama kupitia VIKOBA na pia suala la mifumo ambalo litarahisisha takwimu kusomana jambo ambalo litarahisisha kuongeza hamasa ya chanjo.

Kwa upande wake, Salome Mwinjuma kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya amesema mtoto asiyepata chanjo anaweza kupata madhara mbalimbali ikiwemo ulemavu wa macho na viungo vingine vya mwili.

Naye mwezeshaji wa mafunzo ya HCD kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Dkt. Joseph Mushi, amesema mfumo umekuwa na mchango mkubwa katika kuleta ubunifu wa utatuzi wa matatizo kwa kushirikisha jamii.

Baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo ya HCD wakiwemo Viongozi wa dini, viongozi wa jamii na wazee wa kimila wamesema ni muhimu jami kutambua umuhimu wa chanjo katika kuleta ustawi wa jamii.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.