Takribani hekta 470 za hifadhi zilizoko
katika Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na
Manyara, zimeathiriwa na moto katika msimu huu wa kiangazi, kati ya hizo
hekta 132 zipo Wilaya ya Same yakiwemo baadhi ya maeneo ya hifadhi ya Msitu
wa asili Chome (Shengena).
Kaimu Kamanda wa Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini Agustine Mathias, ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa
mafunzo ya ufuatiliaji moto katika hifadhi za misitu, yanayolenga kuimariusha
utayari wa TFS katika kudhibiti matukio ya moto kwenye Hifadhi za Mazingira Asilia,
Hifadhi za Misitu na Misitu ya Kupandwa.
Amesema miongoni mwao sababu za
matukio ya moto ni pamoja na kuwepo kwa imani potofu kwamba baadhi ya watu ambao wanashindana kuchoma moto
na yule ambaye moto wake utaenda mbali anaonekana ataishi muda mrefu kuliko
wenzake.
Sababu nyingine aliyoitaja ni
kuweko kwa shughuli za kijamii, ikiwemo uandaaji wa mashamba, uvunaji holela wa
asali, uchomaji mkaa na uwindaji wa wanyama pori nazo pia ni sababu zinachangia
kuweko kwa majango ya moto.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Same Kasilida Mgeni, alionya wananchi kuacha mara moja tabia ya kueneza imani
hizo potofu kwa jamii, huku akisisitiza kwamba Serikali haitasita kuchukua
hatua kali kwa mtu yeyote atakayebainika kuendekeza vitendo hivyo kwani
vinasababisha uharibifu wa mazingira.
“Haya mafunzo yamekuja wakati muafaka nimekuwa nikitembea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya yangu ya Same, kati ya jambo ambalo limekuwa likichefua sana ni kuona namna wananchi wakichoma moto ovyo jambo ambalo linaharibu mazingira yetu ikiwemo maeneo yetu haya ya hifadhi.” Amesema DC Kasilida.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza Serikali kuendelea kuchukua hatua za
kukabiliana na watu wanaoharibu mazingira kwa kuchoma moto, ambapo pia ameomba jitihada
za pamoja kati ya Serikali ya Wilaya na taasisi za uhifadhi zinahitajika ili kuhakikisha
wahusika wote watakaobainika kuharibu mazingira wanachukuliwa hatua ili misitu
hiyo iendelee kubaki salama.
Katika hatua nyingine mkuu huyo
wa Wilaya alielekeza kwa TFS pindi kunapotokea matukio ya moto ni vema wakashirikiana
na vyombo vya usalama, likiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuongeza nguvu katika kuokoa sehemu ya
mazingira dhidi ya majanga hayo.
