MOSHI-KILIMANJARO.
Serikali mkoani Kilimanjaro, imewataka Waandishi Waendesha Ofisi (TAPSEA)
kwenye ofisi mbalimbali mkoani humo, kuhakikisha kwamba wana kuwa daraja la
kuunganisha Viongozi na Watumishi wa Umma kwa kuwa wao ndio vioo vya ofisi.
Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Yusuph Nzowa, amesema hayo Novemba
9, 2024, wakati akizindua chama hicho,
hafla iliyofanyika katika ukumbi wa
Ofisi ya Mkuu wa mkoa humo.
Nzowa amewataka TAPSEA hao, kutumia nafasi zao kama njia mojawapo ya
kuboresha utendaji kati ya viongozi na watumishi wa umma kwa kuhakikisha mawasiliano
baina yao na serikali yanakuwa ya wazi
na yenye tija, kwa kuwa wao ndio wanakutana na viongozi mara nyingi zaidi
kuliko watumishi wengine.
“Waandishi Waendesha Ofisi, wanapokuwa makini katika utendaji kazi wao,
watasaidia sana kuwa daraja kubwa na kiungo
muhimu kwa viongozi na watumishi wa umma, kwani kwa kufanya hivyo watafanikisha
kuleta utulivu, amani, katika ofisi.”amesema Nzowa.
Aidha amesema bila kuwa Waandishi Waendeshaji Ofisi katika taasisi yoyote
ile, taasisi hiyo lazima itapwaya kutokana na umuhimu wao na kuwapongeza kwa
kuanzisha chama hicho ambacho kitakwenda kuwa na manufaa makubwa katika mkoa
huo.
Akisoma risala kwa mgeni rasimi Ofisi
Michael Sedekia, amesema lengo la kuwa na umoja huo ni kuweza kutoa huduma kwa
uaminifu, bila kujali muonekano wa mgeni au mwananchi na hivyo kuunga
mkono juhudi za Rais Samia Suluhu
Hassan katika juhudi zake za kuhakikisha kwamba kila mtanzania anapata huduma inayostahili
na kwa wakati.
Aidha amesema TAPSEA mkoa wa Kilimanjaro ina jumla ya Wanachama 145
ambao wametoka katika Ofisi za Serikali na Taasisi mbalimbali za umma na binafsi,
huku akiwahamasisha Waandishi Waendesha
Ofisi wengine ambao hawajajiunga na chama hicho kujiunga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAPSEA
mkoa wa Kilimanjaro Laura Kessy, amesema malengo ya kuanzisha muunganiko huo wa
Waandishi waendesha ofisi mkoa wa Kilimanjaro utasaidia kuwa karibu na kuweza
kupambana na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi.
Chama cha waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) kilianzishwa
mwaka 2008, ili kuandaa, kudumisha, kutekeleza, kulinda haki, kuwasilisha na
kusimamia shughuli zote zinazo husika na waandishi waendesha ofisi mTanzania
Bara na Visiwani.