WAZIRI Mkuu Kassim
Majaliwa amezielekeza Wizara za Elimu Sayansi na Teknolojia na ile ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuendelee kukamilisha mchakato wa
usambazaji wa vitabu kwenye shule zote za msingi, sekondari na vyuo ili somo la
historia na maadili ya mtanzania lianze kufundishwa ifikapo Januari mwaka 2025.
Waziri Mkuu Majaliwa
ametoa maelekezo hayo mnamo Oktoba
26,2024, wakati akifunga mafunzo maalumu
ya Awali ya Uchunguzi kwa Maofisa Wapya 436 Wachunguzi na Wachunguzi Wasaidizi
wa Takukutu yaliyofanyika katika shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro
“Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tamisemi, iendelee kukamilisha
mchakato wa usambazaji wa vitabu kwenye shule zetu, ili somo la historia na
maadili ya Mtanzania lianze kufundishwa ifikapo mwezi Januari 2025.”amesema.
Ameongeza kuwa “Sera mpya inaeleza lengo la Serikali ni kujenga kizazi chenye maadili na uzalendo na chenye kuchukia rushwa.”
Aidha ameitaka Takukuru iendelee
kuongoza ufuatiliaji na usimamizi wa karibu wa fedha zinazotolewa na serikali
kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali, pamoja na fedha zinazotolewa na
taasisi binafsi kwenda kwa wananchi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo. “Wabadhilifu wa fedha za maendeleo waainishwe,
wabainike na waendelee kuchukuliwa hatua zinazostahiki, nilipata ziara ya
kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya, niliyakuta
haya, lakini nashukuru sana maeneo yote niliyopita nilipata ushirikiano mzuri kutoka
kwenye taasisi yetu ya Takukuru, kupitia makamanda wa wilaya na mikoa hongereni
sana."
Aidha Waziri Mkuu
amewahakikishia Watanzania kuwa Seriakli itaendelea kuwa dhidi ya wala rushwa, itaendelea
kuwa wakali dhidi ya idara za ununuzi zinazochepusha fedha za maendeleo.
“Makamand nendeni mkawe
wakali dhidi ya Watumishi wa umma wanaopindisha matumizi ya fedha za miradi
zinazopelekwa na serikali kwenye maeneo ya wananchi.”amesisistiza. Kuhusu wahitimu hao, Waziri Mkuu Majaliwa
amewataka kwenda kufanya kazi kwa weledi, huku wakizingatia Sheria na kanuni
zinazohusiana na shughuli zao huku wakishirikiana na wananchi wenye nia njema
na nchi yetu.
Awali akitoa taarifa za
taasisi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini
(Takukuru) Crispin Chalamila amesema jumla ya watumishi wapya wa taasisi hiyo
436 wamehitimu mafunzo hayo ya awali ambayo amesema ni ya lazima kwa maofisa
wapya wanaojiunga na taasisi hiyo.
Akimkaribisha Waziri
Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, George Simbachawene, amewataka wahitimu hao kujituma wakati wakitekeleza
majukumu yao ili kuakisi juhudi kubwa
zinazofanywa na Serikali katika kuiimarisha Takukuru ikiwemo kwa
kuipatia vitendea kazi na kuongeza nguvu kazi kupitia ajira mpya.
Wakati wa halfa hiyo,Waziri Mkuu aliukabidhi uongozi wa Takukuru magari mapya 88 ambayo yatasambazwa nchini kote, hayo yakiwa ni sehemu ya magari zaidi ya 195 ambayo Serikali imeyaagiza ili kuiimarisha taasisi hiyo.