Wanafunzi wa shule ya sekondari TPC wajengewa bweni, maktaba na FT-Kilimanjaro

MOSHI-KILIMANJARO

Elimu ni jambo la muhimu sana ambalo huchochea maendeleo ya watu binafsi na ya nchi kwa ujumla, pamoja na umuhimu wake huo sekta ya elimu, imekubwa na changamoto mbalimbali hususani kwa watoto wa kike

Moja wapo ya changamoto hiyo ni watoto kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni hasa kwa wanafunzi wa kike wanaosoma shule za sekondari, ambao wamekuwa wakikumbana na vishawishi vingi, vinavyopelekea kwao kukatisha masomo yao

Akizungumza Gladness Kimaro, mwanafunzi wa shule ya sekondari TPC anasema, mara nyingi amekuwa akikatishwa tamaa ya kusoma kutokana na kutembea umbali wa kilometa 12 na kutawaliwa na hofu ya kuadhibiwa na mwalimu kwa kuchelewa kufika shuleni baada ya kutembea muda mrefu.

“Mradi huu wa bweni kwa wanafunzi wa kike ambalo tumejengewa na Shirika la FTK, limetusaidia sana kutupunguzia changamoto ya kutembea umbali mrefu.”amesema.

Mwanafunzi mwingine  wa kidato cha pili Esther Edgar shule ya sekondati TPC anasema umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni ni kulometa 10, ilikuwa inapelekea changamoto ya kuchelewa kufika shulenina hivyo kupoteza vipindi na ufaulu wake kushuka.

Elisipegwa Kitundu mwanafunzi wa kidato cha tatu, amesema alikuwa analazimika kutembea umbali wa kilometa 15 kutoka kijiji cha Kikavu hadi shuleni.

Amesema kabla ya kujengwa kwa bweni hilo, alikuwa hafanyi vizuri kitaaluma kwenye masomo yake kutokana na kufika akiwa amechoka na hivyo kushindwa kujisomea

Mwanafunzi wa kidato cha nne Liliani John, amesema alikuwa akitoka nyumbani saa kumi na moja alfajiri na kufika shuleni saa tatu asubuhi kutokana na changamoto ya usafiri, ambapo usafiri ambao ulikuwa unapatikana ni malori ya kubeba mchanga, wakati mwingine wanakataa kukubena na wengine wanapombeba wanamtaka kingono.

Kwa kutambua changamoto hizo Shirika lisilokuwa la Kiserikali kutoka nchini Uholanzi lililoko mkoani Kilimanjaro (FTK) limekabidhi miradi miwili ya maendeleo kwa wakazi wanaozunguka Kiwanda cha Sukari TPC, kilichopo Wilaya ya Moshi Vijijini ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi bweni na maktaba kwa shule ya shule ya sekondari TPC Meneja Huduma za Jamii wa Kiwanda cha Sukari TPC na Msimamizi wa Shirika la FTK Lazaro Urio, amesema shirika hilo limekabidhi miradi miwili ya maendeleo ikiwemo bweni la watoto wa kike pamoja na maktaba kwa shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Urio amesema FTK kwa kushirikiana na Kiwanda cha Sukari TPC wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja ili kupunguza changamoto hizo kwa kutekeleza na kutengeneza mazingira rafiki, salama na wezeshi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuchochea upatikanaji wa elimu bora na maendeleo ya nchi kwa ujumla

Amesema ujenzi wa bweni umegharimu kiasi cha Sh milioni 147, ambapo lina uwezo wa kuchukua watoto 64 wa kike huku ujenzi wa maktaba ukigharimu kiasi cha Sh milioni 126, ambayo ina uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 48.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya FTK, Jaffary Ally, amesema taasisi hiyo inatumia zaidi ya Sh bilioni 1 kila mwaka kwa ajili ya huduma za jamii katika Wilaya za Moshi Vijijini, Hai mkoani Kilimanjaro, pamoja na Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Kuhusu ujenzi wa bweni hilo Ally, amesema watoto wengi wa kike walikuwa wakirubuniwa kwa zawadi ndogo ndogo, au kubakwa na watu wenye nia mbaya jambo ambalo liliwaweka kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa au kupata mimba na kufukuzwa shule.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya TPC Salehe Mwijuma Shekibwai, amesema awali wanafunzi hao walikuwa na changamoto nyingi ikiwemo ya kutembea umbali mrefu na kwamba kujengwa kwa bweni hilo na maktaba, imeleta manufaa makubwa sana kwa wanafunzi hao.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.