MOSHI-KILIMANJARO
Zaidi ya wanafunzi 1,000 wa kata zilizoko
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC) na ambazo ziko jirani na Kampuni ya
kutengeneza Sukari ya TPC Limited ya mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wamekwepa
adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, baada ya uanzishwaji
wa shule mbili za Sekondari katika eneo la TPC Ltd.
Hayo yamesemwa Oktoba 25, 2024 na Msimamizi wa
Shirika lisilo kuwa la Kiserikali la FTK Lazaro
Urio, wakati wa hafla ya kukabidhi Mabweni na Maktaba kwa shule ya Sekondari
TPC, ambayo ni kitengo cha uwajibikaji kwa Jamii (CSR) cha Kiwanda cha Sukari TPC
iliyofadhili ujenzi wa shule, mabweni na miradi ya maktaba.
“Kabla ya ujenzi wa shule hizo, wanafunzi
wengi wao wakiwa ni watoto wadogo walilazimika kutembea umbali mrefu kufika
shule zilizo nje ya eneo la TPC”, alibainisha na kuongeza, ndipo wazo la
kuanzishwa kwa shule mbili za sekondari za TPC na Shule ya Sekondari ya
Chewe katika eneo hilo ilianzishwa.
Urio amesema kuwa, baada ya kujengwa
kwa shule hizo mbili, changamoto nyingine iliibuka ambapo amesema, safari hii
wanafunzi wengi kutoka nje ya eneo la TPC walilazimika kutembea umbali wa
kilomita 14 hadi 20 kwenda na kurudi kutoka katika shule hizo mbili.
"Ili kukabiliana na changamoto hiyo,
FTK ilikuja na wazo lingine la kulipia usafiri wa wanafunzi kwa kukodisha
mabasi, ambapo wazazi walialikwa kuchangia asilimia 50 ya gharama, lakini wengi
hawakuweza kufanya hivyo kwa sababu mbalimbali", amesema.
Kwa mujibu kiongozi huyo, kufuatia
changamoto hiyo mpya FTK ilikuja na wazo la ziada la kujenga bweni katika shule
ya Sekondari ya TPC litakalohifadhi wanafunzi 64 waliokuwa wakitembea umbali
mrefu kwenda na kurudi shule ya sekondari ya TPC.
“FTK iliamua kuwekeza katika shule ya Sekondari
ya TPC kwa kujenga bweni jipya lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 64
kwa gharama ya shilingi milioni 147, ambapo uongozi wa shule ulipewa
jukumu la kuweka vitanda kwa ajili ya bweni hilo”, amesema Urio.
Kuhusu maktaba mpya ya shule hiyo, Urio amesema
ujenzi wake umegharimu Sh milioni 126 na kwamba itajumuisha maabara ya
kompyuta.
“Maktaba hii haina samani hivyo nitoe rai
kwa wadau mbalimbali kuungana na FTK kukusanya jumla ya Sh milioni 25 ili kumudu
gharama za samani zote zinazohitajika katika maktaba hiyo mpya”, amesema.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya FTK, Jaffary Ally, amesema taasisi
hiyo inatumia zaidi ya Sh bilioni 1 kila
mwaka kwa ajili ya huduma za jamii katika wilaya za Moshi Vijijini na Hai
zilizoko mkoani Kilimanjaro, pamoja na Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Wadau wa Maendeleo kutoka Uholanzi, wakiwa katika eneo la shule ya Sekondari TPC
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari TPC wakiwa wanajisomea
Jengo la Maktaba lililogharimu kiasi cha Sh milioni 126, ambalo lina uwezo wa kutumiwa na Wanafunzi 48.
Bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 64 wa kike limejengwa na Taasisi isiyo kuwa ya kiserikali ya FT-Kilimanjaro na kugharimu kiasi cha Sh milioni 147.