MWANGA-KILIMANJARO
Mbunge wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro Joseph Tadayo ametoa wito
kwa Watanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ili kukuza utalaii wa
ndani, badala ya kutegemea watalii kutoka nje ya nchi.
Ametoa wito huo Oktoba 27/2024, wakati akizungumza na Waandishi wa
habari mjini Moshi, kuhusu namna ya kukuza sekta ya utalii nchini hususani
utalii wa ndani.
“Sekta ya utalii hapa nchini ikiwemo wilaya ya Mwanga inaendelea kukua
siku hadi siku kwa kupitia maono ya rais Samia Suluhu Hassan hasa kwa kupitia filamu
yake ya Royal Tour,” amefafanua Tadayo.
Mbunge huyo ameendelea kusema kuwa, Wilaya ya Mwanga kwa kushirikiana
na Wadau Utalii, imeandaa Tamasha Maalumu la kukuza Utalii ikiwemo Mbio Maalumu
ya Mwanga Festival and Marathon 2024 ambayo itayofanyika mwezi Desemba 27 mwaka huu.
“Mbio hizo zitakuwa za kilometa tano, zitaanzia uwanja wa Cleopa Msuya
na kutamatika katika Gereza la Kilulu na nitumie nafasi hii kuwashukuru wadau
mbalimbali wakishirikina na halamashauri ya wilaya ya Mwanga kufanikisha
Tamasha hili ikiwemo familia ya Mberesero kupitia kupitia taasisi ya Kisangara Tours,” amesema
Tadayo.
Ameendelea kufafanua kuwa, Mbio hizo zitakuwa na faida nyingi sana katika
kukuza sekta ya utalii, hususani utalii wa ndani katika wilaya ya Mwanga na hivyo
kukuza uchumi.
Amesema wilaya ya Mwanga ina vivutio vingi vya utalii ambavyo
havitangazwa sana na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi
wa rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga mazingira rafiki ya uwekezaji ambapo
sekta binafsi zimevutiwa sana kuwekeza kutokana na utendaji wake mzuri.
“Katika wilaya yetu ya Mwanga kuna vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo
havijatangazwa sana ikiwemo Jiwe linaloitwa ‘Mkumbavana’ ambapo watoto
walipokuwa wakizaliwa na changamoto ikiwemo ya ulemavu walikuwa wakipelekwa na
kutupwa na kufia huko ambapo Wajerumani walipokuja walianza kuwaelimisha watu na
kuacha tabia hiyo.” amefafanua mbunge huyo.
Pia Tadayo aliendelea kufafanua kuwa, Mtunzi asilia wa wimbo wa maarufu
wa Kizalendo wa ‘Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote, ulitungwa na
Mchungaji Sila Msangi mzaliwa wa Kata ya Kifula Wilayani humo.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Munkunda ametoa
wito kwa wananchi wa wilaya ya Mwanga kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo
maalumu.
“Pia ninatoa wito kwa wana-Mwanga wanaoishi Ughaibuni (Diaspora) pindi
watakapokuja kujumuika na familia zao katika sikuu za mwisho wa mwaka kushiriki
katika tamasha hilo,” amesisitiza mkuu huyo wa wilaya.