Majaliwa;Takukuru ongezeni kasi ya kudhibti rushwa kwenye ukusanyaji wa mapato, manunuzi ya umma, ugawaji ardhi, utoaji wa huduma za jamii

MOSHI-KILIMANJARO.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kuongeze kasi na mikakati ya kudhibiti rushwa hasa katika maeneo ya ukusanyaji mapato, manunuzi ya umma, michakato ya ajira katika utumishi wa umma, mifumo ya ugawaji wa ardhi pamoja na kwenye eneo la utoaji wa huduma za jamii.

Waziri Mkuu  Majaliwa amesema hayo, Oktoba 26, 2024 wakati akifunga mafunzo ya Awali ya Uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), yaliyofanyika kwenye Shule ya Polisi Tanzania (TPS-Moshi) Moshi mkoani Kilimanjaro.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ameielekeza Takukuru kuongeza ufuatiliaji na usimamizi wa karibu wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya  maendeleo.

Amesema ziko fedha ambazo zimekuwa zikitolewa taasisi binafsi,  kwenda kwa wananchi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akiitaka taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini Takukuru kuhakikisha wabadhilifu wa fedha hizo wanapaswa kubananishwa na kuchukuliwa hatua stahiki pasipo upendeleo wa namna yeyote.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza Takukuru kuweka nguvu kubwa katika eneo la chaguzi zinazoendelea, kwani kuna baadhi ya watu ambao wanataka kuingia madarakani kwa njia za rushwa, hivyo Takukuru  inao wajibu wa kwenda na kufuatilia namna ya mwenendo wa uchaguzi unakwenda.

Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amemshukuru Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa alioufanya ikiwemo ununuzi wa magari, ujenzi wa majengo katika ofisi za Takukuru wilaya na mikoa.

Kuhusu ajira za maafisa uchunguzi hao Waziri Mkuu amesema kuwa maofisa hao  watakwenda kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Takukuru imepatiwa jumla ya Sh bilioni 30 za kununulia magari 195 ambapo magari 88 yameshanunuliwa.

Awali akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Takukuru Ayoub Akida amesema kuwa jumla ya washiriki waliohitimu mafunzo hayo ni 436, ambapo wanawake ni 175 na wanaume 261.

Amesema wahitimu hao wamegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza ni la Maafisa Uchunguzi 323, wanaume wakiwa ni 182 na wanawake 141, na kundi la pili ni la Wachunguzi Wasaidizi 113, wanaume wakiwa ni 79 na wanawake ni 34.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa wahitimu ambao ni waajiriwa wapya wa Takukuru, kutekeleza majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.