PBWB waanza kuondoa tope lililokuwa limejaa kwenye mto Rau

MOSHI-KILIMANJARO

Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani (PBWB) umeweka mikakati inayolenga kuzuia uvamizi wa Mto Rau ili pamoja na mambo mengine kuzuia mafuriko ambayo huathiri watu wakati wa mvua.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani (PBWB) Mhandisi Segule Segule, alipotembelea na kukagua usafishaji wa mto Rau unaoendelea, baada ya mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka huu kuathiri familia nyingi katika kata za Mji Mpya na Msaranga Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Amesema kuwa PBWB pia imepanga mikakati itakayopelekea kulinda mto huo dhidi ya uchafuzi wa mazingira kwa sababu kuna watu wamegeuza mto huo kuwa sehemu ya kutupa takataka.

"Huu ni mto ambao maji yake yanatumiwa na binadamu hivyo uchafuzi wake unaweza kuleta madhara ya kiafya hivyo ni vyema tukazuia athari zisitokee”, amesema.

Akizungumza katika ziara hiyo Diwani wa Kata ya Mji Mpya Abuu Shayo, ameishukuru Serikali kupitia uongozi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) kwa kuchukua hatua ambazo amesema zitaepusha mafuriko wakati wa mvua siku zijazo.

“Mafuriko yaliyotokea Aprili 24 mwaka huu, yaliathiri jumla ya kaya 690 katika Kata mbili za Mji Mpya na Msaranga, wengi wao walipoteza kila kitu baada ya mali zao kuchukuliwa na maji na mtu mmoja kufariki dunia, ni matumaini yangu baada baada ya kazi hii madhara kama haya hayatatokea tena," amesema Diwani Abuu.

Aidha ametoa wito kwa uongozi wa (PBWB) kuweka alama za mipaka (beacon) zitakazoonyesha mipaka inayotenganisha makazi ya watu na eneo lililotengwa ili kuepusha uvamizi. 

"Kuna watu wanaodai kuwa maeneo ya karibu na mto Rau ni mali yao wakati dalili zote zinaonyesha eneo hilo limehifadhiwa; uamuzi wa kuweka alama hizo za mipaka utaondoa utata", amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Msaranga, Dkt. Charles Lyimo, amesema kuwa ukosefu wa mipaka kati maeneo ya mto na makazi umesababisha watu kuingia katika maeneo yasiyokubalika na kufanya shughuli za kibinadamu zinazoathiri mazingira ya mto Rau.

“Watu hawa wanafanya shughuli za kilimo zinazoathiri mazingira ya mto Rau ambapo misimu ya mvua inapofika, mto hufurika na maji kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara mengi”, amesema.







 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.