Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mbio za Mwanga Festival Marathon Frida Mberesero, akizungumzia mbio hizo zitakazo fanyika Desemba 27, 2024 wilayani humo, ambazo zitakwenda sambamba na Tamasha la Utalii Wilayani humo (Mwanga Tourism Festival).
MWANGA-KILIMANJARO
WAKATI wa serikali
ikiwa imedhamiria kuhakikisha idadi ya watalii wanaoingia hapa nchini
inaongezeka na kufikia milioni tano fikapo mwaka 2025 kutoka milioni 1.8 ya sasa, kumekuwa na mikakati mbalimbali
inayofanywa na Serikali pamoja na Wadau wengine katika Sekta ya Utalii hapa
nchini.
Mikakati hiyo ikiwemo
ule uliotekelezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo kwa kushiriki
kutengeneza filamu ya Royal Tour, nchini Tanzania imeanza kuzaa matunda
kutokana na idadi ya Watalii kuanza kuongezeka.
Mikakati hiyo imekua
chachu kwa wadau wengine nao kujitokeza na kuanza kufanya kampeni ambazo
zitachangia ongezeko hilo ili kuendelea kuongeza mapato ya Serikali kuptia
Sekta ya Utalii hapa nchini.
Moja wapo ya mikakati
hiyo ni ule ambao unaandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro
kwa ushirikiano na Kampuni ya Waongoza Watalii ya Kisangara Tours.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Maandalizi ya Matukio hayo Frida Mberesero, anasema kuwa mkakati huo
utahusisha uanzishwaji wa Mbio za nyika Wilayani humo zitakazojulikana kama
Mwanga Festival Marathon, ambazo zitakwenda sanjari na Tamasha la Utalii Wilayani humo (Mwanga
Tourism Festival) matukio ambayo anasema yatakuwa yanafanyika kila mwaka.
“Madhumuni ya kuanzisha
matukio haya mawili ni kuitangaza Wilaya ya Mwanga na vivutio vyake vya utalii,
lengo kuu likiwa ni kupeleka ujumbe ya kuwa viko na hivyo kuvutia watalii wengi
zaidi kutoka ndani na nje ya nchi”, anasema.
Frida ambaye pia ni Mkurugenzi
wa Kisangara Tours, anaendelea kusema kuwa mkakati huo mbali na uongozi wa
Serikali pamoja na Wadau wengine wa Utalii walioko Wilayani humo, pia
utawahusisha wananchi wengine wa wilaya ya Mwanga walioko ndani na nje ya nchi
(diaspora) ili kuhakikisha linafanikiwa na hivyo kutimiza azma ya kuitangaza Wilaya
ya Mwanga.
“Tamasha hili litakuwa
linafanyika Desemba ya kila mwaka, kutokana na kuwa katika kipindi hicho cha
mwaka watu wengi huwa wako kwenye mapumziko hivyo litawavutia watu wengi kutoka
ndani na nje ya Wilaya ya Mwanga”, anasema Mkurugenzi huyo.
Anaendelea kusema kwamba
Mwanga Marathon itakuwa ikifanyika tarehe itakayokuwa imepangwa Desemba 27,
mwaka huu, na kufuatiwa na Tamasha la Mwanga Tourism Festival, ambalo
litafanyika kwa siku mbili mfululizo baada ya Marathon kufanyika.
“Kwa kuanzia, Mwanga
Marathon inatarajiwa kufanyika Desemba 27, mwaka huu na kufuatiwa na Festival
itakayofanyika kwa siku mbili, Desemba 28 na 29, mwaka huu”, anasema.
“Mbio za Mwanga
Marathon zitafanyia katika uwanja wa Cleopa Msuya, ambapo washiriki watakimbia
kwa kilomita 5, kutoka uwanja wa Cleopa Msuya hadi eneo la gereza la Kilulu,
ambapo pia washiriki wanaweza kufanya hivyo kwa kutembea”, anasema na kuongeza,
mipango ya baadaye ni kuwa na mbio za kilomita 21.
Anaongeza, “Baada ya
hapo, Mwanga Tourism Festival itafuata siku ya Desema 28 na 29 ambapo
linatarajiwa kufanyika eneo la Bwawa ya Nyumba ya Mungu lililoko Mwanga”.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Athuman Munkunda anasema kuwa uongozi wa
Serikali Wilayani humo umejipanga ili kuhakikisha vivutio vya utalii vilivyoko
wilayani humo vinatangazwa ili kukuza Uchumi
wa wilaya hiyo kupitia Sekta ya Utalii.
“Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan, ametuonyesha njia kupitia filamu yake ya Royal Tour Tanzania;
filamu hiyo ni dibaji; baada ya kutengeneza filamu hiyo na uzinduzi wake,
alitoa maelekezo kwa viongozi wote kuhakikisha wanakuja na mikakati inayolenga
kutangaza vivuyio vya utalii vilivyoko maeneo yao; mkakati wetu huu unalenga
kutekeleza agizo hilo”, anasema DC Munkunda.
Anasema “Wilaya ya
Mwanga inavivutio vingi vya utalii, ikiwemo Bwawa la Nyumba ya Mungu, Ziwa
Jipe, Ngoma za Kipare na Utamaduni wa kabila la Kipare kwa ujumla ambavyo
vikitangazwa ipasavyo na kupitia mbio hizo Wialaya yetu itakuwa ikipokea wageni
wengi kutoka ndani na nje ya nchi kila mwaka na hivyo kukuza Uchumi wa wilaya
ya Mwanga.”anasema.
Naye Katibu wa Kamati
ya Maandalizi ya matukio hayo Zawadi Mirambo, anasema kuwa maandalizi ya mbio hizo
na Tamasha hilo yamefikia asilimia 60, na kutoa wito kwa wanaotarajia kushiriki
mbio na tamasha hilo kujiandikisha.Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bi, Mwanahamisi A. Munkunda, akizungumza na waandishi wa habari hawapo katika picha juu ya mbio za Mwanga Festival Marathon zitakazo fanyika Desemba 27, mwaka huu wilayani humo.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya matukio hayo Bi. Zawadi Mirambo, akizungumzia maandalizi ya mbio hizo na Tamasha la Utalii.