Mkuu wa wilaya ya Mwanga Bi. Mwanahamisi A. Munkunda, akizungumzia mbio za Mwanga Festival Marathon zitakazofanyika Desemba 27, 2024.
MWANGA-KILIMANJARO
Serikali Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, kwa kushirikiana na Wadau wa utalii wameanzisha mbio za nyika Wilayani humo, zitakazojulikana kama Mwanga Festival lenye lengo la kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya hiyo Mwanahamisi Munkunda, ameyasema hayo Oktoba 24,2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake, kuhusiana na tukio hilo ambalo litafanyika Desemba 27 mwaka huu, lengo likiwa ni kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika wilaya hiyo.
Munkunda amesema miongoni mwa maeneo yenye vivutio vya utalii vinavyo patikana wilayani humo, katika Nyanda za Juu Kaskazini (Noth Pare) ni pamoja na maeneo ya kihistoria kama vile Msitu wa Kindoroko pamoja na Mlima Kindoroko, ulioko upareni.
“Wilaya ya Mwanga tunavyo vivutio vingi vya utalii, ambavyo vingi havijatangazwa vya kutosha, kuna Utamaduni wa Wapare, ambao wanapatikana Usangi, Ugweno, Kisangara Juu (Ngujini) Utalii wa Elimu, ikiwemo shule ya kwanza ya middle school aliyosoma Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya na Mwashamu wa kwanza (Home of Catholic Church) Josephat Lobulu.”amesema.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema pia kuna utalii wa kuabudu, ukiwemo misikiti ya kwanza iliyojengwa Usangi na ugweno, Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT) linalopatikana Usangi, na Kanisa la Roman Catholic lililopo Kilomen.
Ameongeza kuwa “Kuna utalii wa jiwe ambalo linafahamika kama ‘Mkumbavana’ Mama alipokuwa akizaa mtoto mwenye ulemavu alikuwa akipelekwa mtoto wake kwenye jiwe hilo na kulazwa hadi anasinzia, akiamka alikuwa akitereza na kuanguka na kuliwa na wanyama wakali.”
Vilevile amesema kupitia tamasha hilo, wananchi watapata fursa ya kutembelea uwanda wa chini, kuna Bwawa la Nyumba ya Mungu, Ziwa Jipe ambako kuna utalii wa kusafiri kwa kutumia mtumbwi na kupiga kasia pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambako wanapatikana wanyama aina ya tembo, faru, mbwa mwitu, twig, nyati na ndege wa aina mbalimbali.
Aidha amewataka wananchi wilayani humo, ambao watakuja kwa ajili ya mapumziko ya mwezi Desemba, kutumia fursa hiyo, kutembelea vivutio hivyo ikiwa ni sehemu ya kutangaza vivutio vilivyopo Mwanga, ili kuwavutia watalii wengi zaidi.
“Katika kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alizindua filamu ya Royal Tour kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii nchini na sisi Wilaya ya Mwanga tumeona matokeo yake chanya hivyo basi kama wilaya tumeamua kumuunga mkono Rais wetu kwa kufanya tamasha hili la utalii, ambalo litaibua fursa za vivutio vingi vya utalii.
Amesema
kupitia mbio hizo zenye lengo la kutangaza utalii wa Mwanga, litakwenga kufungua
fursa kwa wawekezaji mbalimbali hapa nchini kuja kuwekeza katika wilaya ya Mwanga.Jiwe la "Mkumbavana" Mama alipokuwa akizaa mtoto mwenye ulemavu alikuwa akipelekwa kwenye
jiwe hilo na kulazwa hadi anasinzia, akiamka alikuwa akitereza na kuanguka kwenye msitu uliokuwa na wanyama wakali.