Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), kimeiomba Serikali kuangalia upya Sera ya Taifa ya Mwaka 2004 inayohusiana na huduma na maendeleo kwa watu wenye ulemavu nchini.
Mratibu wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) Kizito Wambura, ameyasema hayo Oktoba 23, 2024 wakati wa ufunguzi wa kongamano la fimbo nyeupe, lililofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kuelekea maadhimisho ya miaka 60 toka kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1964.
Wabura amesema kutokana na mabadiliko ya Sayansi na teknolojia duniani, kuna mabadiliko mengi ambayo yamejitokeza hivyo kuna haja ya kufanyiwa mapitio sera hiyo ili kuweza kwendana na wakati.
“Sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 imepitwa na wakati, hivyo inatakiwa kufanyiwa mapitio ili iendane na wakati kwa kuzingatia mkakati wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu wa mwaka 2006, kwani toka mwaka 2004 hadi sasa ni miaka 20, yako mabadiliko mengi sana yamejitokeza duniani ya Kisayansi, teknolojia, ni lazima tufikie hatua ya kuifanyia mapitio ya sera hii.”amesema wambura.
Amesema TLB haiwezi kufanya hayo, pasipo kupata mawazo kutoka kwa wadau TLB, ikiwa ni sambamba na kupokea maoni yao kama wadau wa Sera hiyo ya Taifa ya huduma na maendeleo kwa watu wenye ulemavu.
Amesema watu wenye ulemavu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupata huduma , jambo ambalo huwakwamisha wengi wao na kuishia kukata tama.
Aidha ameongeza kuiwa “Mustakabali kwa wasioona katika kufanikisha miundombinu ya jumuishi, hatuhitaji kukutana na vikwazo katika ufikivu wetu au ujongevu kwenye maeneo ambayo tunakwenda kutoa huduma kwa jamii,”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) Habiba Salumu Ngulangwa, amesema kongamano hilo pia litajadili mwelekeo wa TLB, afya ya akili kwa watu wenye ulemavu wa machopamoja na changamoto zake na namna wanavyoweza kuzitatua, upatikanaji wa ajira kwa watu wasioona.
Akizungumza mmoja wa washiriki wa kongamano hilo Mwalimu Mussa Mashauri, amesema kuwa suala la umasikini imekuwa ni changamoto kubwa kwa watu wasioona kupata ajira.
“Bado mtizamo kwa wasioona kwenye jamii yetu sio mzuri sana, lakini pia changamoto ya umasikini na ajira, kwa kulitambua hilo kamati ya utendaji ya TLB tanzania imejipanga kwenda kutatua changamoto hizi kwa kuanzia na uboreshaji wa matawi ili yaweze kujitegemea kiuchumi, kuanzia ngazi za wilaya, mikoa na taifa kwa ujumla.
Kongamano hilo limewashirikisha Maafisa Ustawi,
Maafisa Elimu Maalumu, Wananchama wa TLB pamoja na Wakazi wa Mkoa wa
Kilimanjaro.


